●   Awasihi Watanzania kuchukua Vitambulisho vyao vya Uraia.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itaanza kuchukua hatua za kuwasajili na kuwatambua watoto walio chini ya umri wa miaka 18, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa utambulisho wa Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hatua hiyo itamuwezesha kila Mtanzania kutambulika kuanzia hatua za mwanzo za maisha yake pamoja na kuondoa pengo lililokuwepo katika mfumo wa utambulisho kati ya mtoto anapozaliwa na anapofikisha umri wa miaka 18.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Septemba 16, 2026, wakati akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

“Mfumo huu utasaidia kupunguza usumbufu wa kutumia nyaraka au vitambulisho vingi wakati wa kupata huduma mbalimbali, kwa kuwa taarifa muhimu za mwananchi zitaendelea kutambulika na kuhifadhiwa katika mfumo mkuu wa Taifa wa utambuzi” amesema.

Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania ambao tayari wamesajiliwa na vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika kwenda kuvichukua, akisisitiza kuwa utambulisho ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Kitambulisho chenyewe kama nchi tumeingia gharama, tumeahirisha baadhi ya shughuli za maendeleo ili tutoe vitambulisho. Lakini tunapokuwa tumetoa kitambulisho, halafu mhusika haendi kuchukua, haya ni mambo ambayo yanakwamisha malengo mapana,” amesema.

Amesema kwa sasa NIDA imeboresha utaratibu wa kuwafahamisha wananchi pale vitambulisho vyao vinapokuwa tayari, ikiwemo kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS), hivyo hakuna sababu kwa wananchi waliokwishaandikishwa kuacha vitambulisho vyao kwa muda mrefu bila kuvichukua.

“Niendelee kusisitiza wananchi wote ambao wako tayari na vitambulisho vyao, basi waende kuvichukua. Lengo letu ni kuona kuwa hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika kupata vitambulisho vya Taifa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho katika mfumo wa utambulisho wa Taifa ili kuhakikisha unakidhi mahitaji ya sasa ya kiteknolojia, usalama wa taarifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Serikali imeendelea kuboresha mfumo wa utambulisho ili kupunguza utegemezi wa vitambulisho vingi kwa huduma mbalimbali na kuelekea katika mfumo ambao taarifa muhimu za mwananchi zinapatikana kupitia mfumo mkuu wa Taifa wa utambuzi,” amesema.

Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema NIDA imefanya mapitio ya jumla ya vitambulisho vilivyotolewa katika ofisi zake na vituo 10 vya usajili vilivyopo katika kila wilaya, bila kuhusisha vituo 156 vilivyotajwa awali.

Amesema hadi sasa jumla ya watu 27,520,835 wamesajiliwa, ambapo watu 23,515,667 wamekwishapatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa. Aidha, vitambulisho 21,526,635 vimezalishwa, huku bado kukiwa na idadi ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa na wananchi waliostahili kuvipata.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema jamii inapaswa kuacha dhana kwamba NIDA ni taasisi inayotoa kadi pekee, kwa kuwa utambulisho wa Taifa ni msingi wa upatikanaji wa huduma na utambulisho wa mwananchi katika maisha yake yote.

Amesema NIDA inaendelea kuboresha kitambulisho cha Taifa ili kiwe cha kidijitali na kiweze kuhusisha taarifa muhimu za huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo cheti cha kuzaliwa, bima ya afya, TIN, leseni ya udereva na taarifa nyingine muhimu, huku taarifa za kiafya kama kundi la damu zikitarajiwa kusaidia wakati wa dharura, kwa kuzingatia uthibitisho wa kitabibu.

Kanji amesema usajili wa watoto tangu wanapozaliwa ni muhimu kwa sababu utamwezesha kila mtoto kutambulika na kupata huduma za kijamii kwa urahisi katika hatua zote za maisha. Amesema zoezi hilo litaanza kwa majaribio katika wilaya za Kilolo, Lungu na Kusini Unguja, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini.