Na Mwandishi Wetu ,Ruvuma,

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesaini mkataba wa ujenzi wa daraja la Luegu lenye urefu wa mita 40.8 na barabara za maungio kwa kiwango cha lami zenye urefu kilometa 2.125 katika barabara ya Naikesi-Kitanda wilayani Namtumbo.

Mkataba huo, umesainiwa jana kati ya TANROADS Mkoa wa Ruvuma na Mkandarasi Kampuni ya Ovans Contruction Ltd na kushuhudiwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini Waziri Homera ameeleza kuwa,ujenzi wa daraja hilo utaondoa kero ya wananchi na adha ya usafiri kutokana na eneo hilo kujaa maji,kusababisha barabara kufungwa na kutopitika pindi mvua zinaponyesha.

Dkt Homera, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha ambazo zinakwenda kuokoa maisha ya wananchi wa kata ya Mgombasi na maeneo mengine katika Wilaya ya Namtumbo kwa kujengwa kwa daraja la kudumu.

Ameipongeza TANRAODS kupata mkandarasi mwenye uwezo mkubwa katika ujenzi wa barabara,na kuwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali na kumpa ushirikiano mkandarasi katika utekelezaji wa mradi huo.

Katika hatua nyingine Waziri Homera alisema,tayari Serikali imeridhia kujenga barabara ya Mtonya-Kitanda kwa kiwango ambayo itakapokamilika itarahisisha shughuli za usafiri na usafi wa mazao kutoka mashambani kwenda mjini kutafuta masoko.

“Jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaonekana na ametoa zaidi ya Sh.bilioni 6 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili na barabara unganishi zenye uregu wa kilometa 2 baada ya miezi 12 kama mkataba unavyotaka,sina wasiwasi na uwezo wa mkandarasi wetu”alisema Dkt Homera.

Kaimu meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ferdinand Mdoe alisema,gharama ya mradi huo ni Sh.bilioni 6.149,983,643 na utatekelezwa kwa miezi 12 na mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema, daraja lililopo limejengwa kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita na wakati wa mvua kubwa maji hufurika na kupita juu,hivyo kukwamisha shughuli za uzalishaji na likapokamilika litapunguza ajali kutokana na kuwa hatarishi hasa kwenye kona za maingilio, chakavu na dhaifu.

Kwa mujibu wa Mdoe, kujengwa kwa daraja jipya katika mto Luegu kutaboresha usafirishaji wa mazao ya kilimo na kibiashara na litakuwa kiunganishi cha huduma muhimu za kijamii.

“kazi zitakazofanyika ni kujenga daraja kubwa lenye urefu wa mita 40.8 kujenga boksi kalavati,kunyayua tuta la barabara upande wa Mtonya,kukata mlima upande wa Naikesi,kujenga barabara za maingilio ya daraja kwa kiwango cha lami,kuweka taa za barabarani 20,mifereji ya kupitisha maji na kuweka alama za barabarani na miundombinu mingine”alisema.

Mdoe alisema,mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na usanifu wa daraja hilo na barabara zake umefanywa na Kampuni ya Luptan Consults Ltd na utasimamiwa na TANROADS-Ruvuma na muda wa utekelezaji ni miezi 12.

Alisema,kutokana na mahitaji ya kibajeti mradi utekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza litajengwa daraja na katika awamu ya pili ni ujenzi wa boksi kalavati,mifereji kwa zege,kujenga barabara unganishi kwa kiwango cha lami,kazi saidizi za barabara kusimika taa na kuhamisha miundombinu na kudhibiti ubora”alisema Mdoe.

Mkandarasi wa mradi huo Valence Urio,amempongeza Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera kutokana na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo na kuhaidi kutekeleza kazi kwa wakati na ubora mkubwa kulingana na makubaliano ya mkataba.

Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ferdinand Mdoe,akimuonyesha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera kulia, mchoro wa  daraja la Luegu linatarajiwa kujengwa upya baada ya daraja lililopo kuchakaa wakati wa  hafla ya kutambulisha mradi wa ujenzi wa daraja hilo lililopo kijiji cha Mgombasi wilayani Namtumbo