*Wakubali jiji lisafishwe, waomba adhabu ziendane na hali ya maisha
*Walalamikia uhaba wa mapipa ya taka, vyoo vya umma
Aziza Nangwa na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Baada ya Serikali mkoani Dar es Salaam kutangaza hatua za kuimarisha usafi, ikiwamo faini ya Sh 300,000 hadi Sh milioni moja kwa baadhi ya makosa ya uchafuzi wa mazingira, wananchi wameibua hofu kuhusu ukubwa wa adhabu hizo.
Wananchi waliozungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wanasema hawaungi mkono uchafuzi wa mazingira, wakitaka utekelezaji wa sheria uende sambamba na kuboresha miundombinu ya usafi pamoja na kutoa elimu.
Wanasema Dar es Salaam inahitaji kuwa safi kutokana na nafasi yake kiuchumi na idadi kubwa ya watu, ingawa jitihada za kufikia lengo hilo zinapaswa kuzingatia pia mazingira ya wananchi wanaotafuta kipato cha kila siku.
Hassami Mwinyi amesema usafi ni muhimu, ingawa kiwango cha faini kinachotajwa ni kikubwa kwa wananchi wenye kipato cha chini.
“Usafi wa jiji ni jambo zuri na hakuna mtu anayepinga. Tatizo ni faini zinazotajwa ni kubwa sana kwa mwananchi wa kawaida. Mtu anayetafuta maisha kwa siku, akipata faini ya milioni moja atapata wapi fedha?” amehoji.
Amesema baadhi ya maeneo bado yanakabiliwa na uhaba wa mapipa na vituo maalumu vya kuhifadhi taka, hivyo wananchi wanapaswa kuwezeshwa kutimiza wajibu kabla ya kuadhibiwa.
Christopher Sheji amesema elimu inapaswa kutolewa kuhusu makosa yanayotozwa faini, viwango vya adhabu na wajibu wa wananchi katika kutunza mazingira.
“Wananchi wengi bado hawajapata elimu ya kutosha kuhusu faini. Serikali ianze kwa kutoa elimu ili kila mtu ajue kosa gani lina adhabu gani na kwa nini,” amesema.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA SEPTEMBA 29 – HADI OKTOBA 5 ,2026


