Na Mwandishi Maalumu – Arusha
30/09/2026 Jumla ya wananchi 621 wakiwemo wanaume 278 na wanawake 343 wamepata huduma za uchunguzi wa saratani katika kambi maalumu iliyofanyika katika Hospitali ya Kaloleni jijini Arusha huku baadhi yao wakibainika kuwa na viashiria vilivyohitaji ufuatiliaji na huduma zaidi.
Kambi hiyo iliyoendeshwa na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Arusha Mjini na Hospitali ya Kaloleni ililenga kusogeza huduma za uchunguzi karibu na wananchi, kutoa elimu kuhusu saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema.
Katika zoezi hilo wagonjwa sita walibainika kuwa na uvimbe kwenye matiti, wawili walikuwa na viashiria vilivyotia shaka kuhusu saratani ya matiti, wanne walibainika kuwa na mabadiliko ya awali kwenye mlango wa kizazi yanayoweza kuhusishwa na saratani huku wagonjwa tisa wakiwa na viashiria vilivyotia shaka kuhusu saratani ya tezi dume.
Kutokana na matokeo hayo jumla ya wagonjwa 16 walipewa rufaa kwa ajili ya uchunguzi na huduma zaidi kulingana na mahitaji yao.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Arusha wakati wa ufungaji wa kambi hiyo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Maguha Stephano alisema wameridhishwa na mwitikio wa wananchi wa waliojitokeza kupata huduma za uchunguzi na elimu kuhusu saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Alisema kambi hiyo haikuwa tu kutoa huduma kwa wananchi bali pia ilikuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano na kujenga uwezo wa wataalamu wa Hospitali ya Kaloleni katika uchunguzi wa awali wa saratani.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kaloleni, Dkt. Laura Urio alisema ushirikiano na ORCI umewezesha wananchi kupata huduma za uchunguzi wa saratani kutoka kwa wataalamu bingwa bila kulazimika kusafiri kwenda mbali.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa zoezi hilo limewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata elimu muhimu kuhusu saratani.



