Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba Serikali kuendelea kulipa kwa wakati madai na stahiki mbalimbali za walimu, ikiwemo fedha za likizo, malipo ya kupanda madaraja na madai mengine ya kiutumishi, ili kuwawezesha walimu kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora.
Ombi hilo limetolewa leo Oktoba 3, 2026, wakati maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yakiendelea jijini Dodoma, ambapo wadau mbalimbali wa elimu wamekusanyika katika mabanda ya maadhimisho hayo katika viwanja vya Nyerere Square kabla ya kuelekea katika eneo maalum la mkutano katika ofisi za CWT.
Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Kusimama pamoja na walimu: Miaka 60 ya kulinda taaluma, kuendeleza hadhi yake na kuunda mustakabali wetu,” huku kilele cha maadhimisho hayo kikitarajiwa kufanyika Oktoba 5, mwaka huu.
Akizungumza baada ya shughuli za kukagua mabanda hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Magesa Protas, alisema walimu wanaendelea kuipenda na kuitendea haki taaluma yao kwa kujitoa kwa moyo katika kuwahudumia wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Alisema CWT imebaini kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili walimu zimeendelea kufanyiwa kazi, ikiwemo masuala ya kupandishwa madaraja na masuala mengine ya kiutumishi.
“Walimu wanaipenda kazi yao na wanajua kuitendea haki kwa kujitoa kwa moyo. Sisi kama Chama cha Walimu tunaendelea kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi ya walimu,” alisema.
Alitaja baadhi ya hatua zinazohusu maslahi ya walimu kuwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya madaraja, stahiki mbalimbali za kiutumishi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Hata hivyo, alisema bado kuna mifumo ya kiutumishi yenye changamoto ambazo zinahitaji kuendelea kufanyiwa kazi ili kumsaidia mwalimu kupata nafuu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa mujibu wa Magesa, malipo ya madai na stahiki za walimu kwa wakati ni muhimu kwa sababu yanamsaidia mwalimu kuwa na utulivu wa kiutumishi na kiuchumi, hivyo kumpa nafasi ya kuzingatia zaidi kazi ya kufundisha, kulea na kujenga maarifa ya wanafunzi.
“Tunaiomba Serikali iendelee kulipa madeni yote ya walimu kwa wakati. Tunaamini mwalimu anapopata stahiki zake kwa wakati anapata nafasi ya kuzingatia zaidi kazi yake na kutoa matokeo chanya katika elimu,” alisema.
Alisema CWT itaendelea kusimama pamoja na Serikali, walimu, wazazi na wanafunzi katika kuhakikisha elimu inaboreshwa, akisisitiza kuwa kazi ya mwalimu si kufundisha pekee bali pia kujenga maarifa, maadili, ujuzi na kuwaandaa wanafunzi kwa maisha na mustakabali wa Taifa.
Magesa pia aliitaka jamii kuendelea kuwaheshimu walimu na kuhakikisha wanapata mazingira salama na yenye heshima yanayolinda hadhi ya taaluma hiyo.
Alisema taaluma ya ualimu ni baraka kwa sababu inamhudumia mwanadamu na ina mchango mkubwa katika kuandaa wataalamu na viongozi wa kesho.
Katika hatua nyingine, CWT imeeleza kuwa itaendelea kujipanga kuwafikia walimu wote nchini ili wawe sehemu ya umoja wa chama hicho na kupata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao kwa pamoja.
TSC YAWEKA HUDUMA KARIBU NA WALIMU
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Maadili na Nidhamu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Asha Kubuva, alisema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa walimu kwa kuwa taasisi mbalimbali zinazowahudumia zimekusanyika katika eneo moja.
Alisema walimu wanaofika katika mabanda hayo hupatiwa huduma, maelekezo na, pale inapohitajika, kusaidiwa kufikishwa katika taasisi au sehemu husika kwa ajili ya kushughulikia changamoto zao.
Kubuva pia alisema maadhimisho hayo yametumika kutoa hamasa kwa walimu kushiriki katika shughuli za kijamii, ikiwemo kuchangia damu kupitia wadau wa huduma ya damu salama.
Alisema uchangiaji wa damu ni muhimu kwa kuwa damu inayotolewa inaweza kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo katika hospitali, hivyo walimu nao wanaweza kutumia nafasi hiyo kuonyesha mchango wao kwa jamii nje ya darasa.
Aidha, aliwataka walimu wenye changamoto za kiutumishi kutoweka mambo hayo kwa muda mrefu, bali kuyawasilisha mapema ili waweze kuhudumiwa kwa wakati na kupata stahiki zao.
“Walimu wenye changamoto wasisubiri hadi hali iwe kubwa. Wawasilishe changamoto zao kwa wakati ili zipate kushughulikiwa na mwalimu aweze kuendelea na majukumu yake ya kuwafundisha watoto vizuri,” alisema.
TSC YAELEZA MAJUKUMU YAKE
Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Ajira na Maendeleo ya Walimu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Magthilde Scapinga, alisema Tume hiyo ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), inayosimamia masuala ya ajira, maadili na maendeleo ya walimu.
Alisema Tume hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi mwaka 2016, ikiwa na Makao Makuu Dodoma na ofisi 139 katika wilaya zote za Tanzania Bara.
Scapinga alisema miongoni mwa majukumu ya TSC ni kusimamia ajira za walimu, kupandisha vyeo, kubadilisha kada kwa walimu wanaojiendeleza kielimu na kuhakikisha walimu wanapata huduma zinazohusiana na utumishi wao.
Alisema Tume pia hushughulikia masuala ya maadili na nidhamu kwa kutoa elimu kwa walimu kuhusu taratibu na kanuni za utumishi, huku hatua za kinidhamu zikichukuliwa kwa watumishi wanaokiuka taratibu.
Aidha, alisema TSC ina jukumu la kushughulikia mchakato wa kustaafu kwa walimu na kusimamia upatikanaji wa stahiki zao kwa wakati.
Scapinga alisema Tume pia ni mamlaka ya rufaa katika masuala ya kinidhamu, ambapo mwalimu asiyeridhika na uamuzi wa mamlaka za chini anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Alisema maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yamekuwa pia fursa ya kuelimisha wananchi na walimu kuhusu majukumu ya TSC na kutofautisha taasisi hiyo na taasisi nyingine zinazohudumia walimu.
Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yanafanyika kuanzia Oktoba 1 hadi Oktoba 5, 2026, huku wadau mbalimbali wakiendelea kutoa huduma, elimu na kusikiliza changamoto za walimu na wananchi katika viwanja vya Nyerere Square, Dodoma.
Siku ya Mwalimu Duniani huadhimishwa Oktoba 5 kila mwaka kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika jamii na maendeleo ya Taifa.








