*Polisi walidai kumkamata kwenye doria, hospitali yasema OCD alimwokota barabarani akiwa taabani kwa kipigo

*Familia yasubiri majibu stahiki ikihoji kukinzana kwa taarifa, huku mwili ukiendelea kuhifadhiwa Bugando zaidi ya mwezi mmoja

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Kifo cha Frank Stanley, aliyefariki dunia baada ya kufikishwa hospitalini akiwa chini ya ulinzi wa polisi mkoani Kagera kimeingia katika sura nyingine baada ya Hospitali ya Mkoa Bukoba kueleza kuwa taarifa ilizonazo zinaonyesha aliokotwa akiwa hajitambui na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD).

Taarifa hiyo imemshangaza baba mzazi wa Frank, Stanley Ndibalema, ambaye kwa muda sasa amekuwa akihoji mazingira yaliyosababisha mwanaye kuishia hospitalini akiwa na majeraha makubwa kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza.

Utata umeongezeka baada ya ripoti za hospitali kueleza historia ya Frank kuwa alishambuliwa na kundi la watu, huku familia ikisema maelezo hayo hayaendani na baadhi ya taarifa ilizopewa awali kuhusu kilichompata.

Mwili wa Frank unaendelea kuhifadhiwa Bugando kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, familia ikigoma kuuchukua kwa maziko ikitaka kwanza ipate majibu ya maswali kuhusu mazingira ya kifo chake.

Awali, familia inadai kuelezwa kuwa Frank alipata matatizo ya kiafya yaliyohusisha sukari na figo, maelezo ambayo imekuwa ikiyapinga ikidai hakuwahi kuwa na historia ya maradhi hayo.

Utata uliongezeka baada ya familia kukabidhiwa taarifa za kitabibu zinazoonyesha Frank alifikishwa hospitalini akiwa na jeraha kubwa kichwani na hali yake ya fahamu ikiwa imepungua.

KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI OKTOBA 6-12, 2026