Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu amehutubia Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) jijini Arusha na kusisitiza kwamba dunia inapaswa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza kwa kuwa hakuna upande unaoweza kufanikiwa bila upande mwingine.
Akizungumza mbele ya Masipika na Wabunge zaidi ya 1,500 kutoka duniani kote, Mheshimiwa Spika amesema kupitia mabunge, tofauti zinaweza kubadilishwa kwa mazungumzo na maslahi yanayopingana yanapatanishwa kupitia hoja.
“Tuna ubinadamu mmoja na hatima ya pamoja. Hatuna tatizo la Kusini mwa Dunia au tatizo la Kaskazini mwa Dunia. Tuna tatizo la kibinadamu. Na linahitaji suluhisho la kibinadamu. Kaskazini ina teknolojia na mtaji, Kusini ina rasilimali, vijana, na ustahimilivu. Hakuna upande unaoweza kufanikiwa bila mwingine.
“Sisi si dunia mbili, sisi ni dunia moja inayojaribu kujenga mustakabali mmoja kwa wanadamu. Madini adimu yaliyo chini ya Afrika na Amerika ya Kusini yanaweza kuendesha mustakabali wa kijani unaobuniwa Ulaya na Amerika. Vijana wa Kusini wanaweza kuendesha uchumi wa Kaskazini,” amesisitiza.






