Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema asilimia 90 ya kero na malalamiko yanayowasilishwa na wananchi mkoani humo yanahusu migogoro ya ardhi, akitoa onyo kali kwa matapeli na madalali wanaojihusisha na uuzaji wa ardhi kinyume cha sheria kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Nyongo amesema migogoro hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi kumiliki ardhi kwa amani na inaweza kuathiri mazingira ya uwekezaji, akisisitiza kuwa Serikali haitawavumilia watu wanaovamia maeneo ya wengine, kuuza viwanja visivyo vyao au kuchochea migogoro kwa manufaa binafsi.
Akizungumza wakati wa ziara yake huko Kisarawe, Bagamoyo na Chalinze, Nyongo alitaja Kibaha na Bagamoyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa migogoro ya ardhi, akieleza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa kuzingatia sheria na haki.
Alisema mpango wa kuanzisha maduka ya ardhi utakuwa miongoni mwa njia za kudhibiti migogoro hiyo, kwa kuweka utaratibu unaowawezesha wananchi wanaotaka kununua au kuuza ardhi kufanya hivyo kupitia mfumo unaotambulika badala ya kutegemea madalali wasio waaminifu.
“Ardhi ni mali, lakini watu wamekuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya wengine, Tunataka migogoro hii ifike mwisho, Tutashughulikia matapeli na wote wanaouza ardhi au viwanja vya watu kinyume cha sheria,” alisema Nyongo.
Nyongo alisema kumekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo yanayohusisha wawekezaji, huku akiwataka viongozi na wananchi kushirikiana kuhakikisha maeneo yanayotengwa kwa uwekezaji yanakuwa na umiliki ulio wazi na mazingira rafiki kwa shughuli za kiuchumi.
Aliwataka wabunge na viongozi wengine kuwasaidia wananchi kupata elimu kuhusu umuhimu wa kulinda maeneo ya wawekezaji na kutatua migogoro kwa njia halali badala ya kuwa vikwazo kwa miradi ya maendeleo.
AWAKEMEA WAFUGAJI
Katika hatua nyingine, Nyongo amewataka wafugaji kuacha mara moja kuingiza na kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima, akisema Serikali haitavumilia uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo.
Alisema maeneo yametengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo kila kundi linapaswa kuheshimu maeneo hayo na kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, badala ya kutumia mabavu na kusababisha hasara kwa wengine.
Aliwataka wakuu wa wilaya kusimamia kikamilifu migogoro ya wakulima na wafugaji na kuhakikisha mtu yeyote atakayebainika kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima anakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema jukumu la Serikali ni kulinda amani na kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaishi kwa kuheshimiana na kufanya shughuli zao bila kuathiriana.
MSATA KUSUBIRI TATHMINI
Kuhusu wananchi wa Msata walioondoka katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kijeshi, Nyongo aliwataka kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi la uthamini litakalorudiwa ili kuwezesha mchakato huo kufanyika kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Baadhi ya wananchi akiwemo Hamis Juma na Amina Shija, walieleza kuwa migogoro ya ardhi na changamoto za wakulima na wafugaji zinaendelea kuwa kero katika maeneo yao.
Juma alisema wananchi waliohusika na eneo la jeshi wamekuwa wakisubiri suluhisho kwa miaka sita bila kupata stahiki zao, akiiomba Serikali kuingilia kati na kuwasaidia.
Kwa upande wake, Shija aliiomba Serikali kushughulikia changamoto ya mifugo katika eneo la Milo ili wakulima waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
BAGAMOYO YAANZISHA OPERESHENI
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa wilayani Bagamoyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga, alisema Serikali imekuwa ikifanya operesheni za kukabiliana na migogoro ya ardhi pamoja na ile inayohusisha wakulima na wafugaji.
Alisema katika operesheni iliyofanyika wiki iliyopita katika Kata ya Fukayose, watu 11 walikamatwa kwa tuhuma zinazohusiana na migogoro hiyo, wakiwemo baadhi ya wafugaji wanaodaiwa kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, viongozi wanaodaiwa kupokea wafugaji na kuwauzia maeneo na wakulima wanaodaiwa kuwakata ng’ombe kwa mapanga bila sababu za msingi.
Ndemanga alisema operesheni za kushtukiza zitaendelea bila kutangazwa mapema ili kuwabaini wanaohusika na migogoro hiyo na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria.





