Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imehitimisha Mpango Mkakati wa Tano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 kwa utekelezaji wa asilimia 82 na kuanza Mpango Mkakati wa Sita wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia, amesema hayo jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2026, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023 hadi 2026/2027.
Akizungumzia mwelekeo wa taasisi hiyo, Kiwia alisema HESLB ina mpango mpya unaolenga kuibadilisha HESLB kutoka taasisi inayojikita katika utoaji wa huduma za mikopo kwenda kuwa Mfuko wa kitaifa wa kugharimia wanafunzi wenye wigo mpana zaidi wa ufadhili.
Aliongeza kuwa HESLB itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika programu maalumu za ufadhili, ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufadhili wa shahada za uzamili wa Mwalimu Julius K. Nyerere Memorial Masters’ Degree Scholarship, pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa wanafunzi wanaosoma masomo yanayohusiana na uhifadhi.
Kiwia amesema mwelekeo huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kupanua fursa za elimu ya juu na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata elimu na mafunzo yanayokidhi mahitaji ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa HESLB itaendelea kuboresha mifumo yake, kuongeza ushirikiano na sekta binafsi na kuimarisha uwazi katika utoaji wa huduma ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wanafunzi.
Akihitimisha, aliomba ushirikiano wa wahariri na vyombo vya habari katika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mikopo ya elimu ya juu, akisema vyombo hivyo vina nafasi muhimu katika kuwaelimisha wanafunzi, wazazi, waajiri na wanufaika kuhusu haki na wajibu wao.
Amesema mafanikio ya HESLB hayawezi kutenganishwa na ushirikiano wa Serikali, vyuo, taasisi za fedha, waajiri, wanafunzi na wadau wengine wa elimu, akisisitiza kuwa kila mkopo unaorejeshwa unatoa nafasi kwa mwanafunzi mwingine kupata elimu.






