Operesheni ya uokoaji inaendelea katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, baada ya jengo refu lililokuwa likijengwa kuporomoka ghafla katika eneo la Eastleigh (ISLII) mchana wa leo.

Mashuhuda wanasema jengo hilo, linalokadiriwa kuwa na takriban ghorofa 18, lilianguka likiwa bado katika hatua za ujenzi, na kuacha kifusi kikubwa katikati ya eneo lenye shughuli nyingi za biashara na makazi.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa huenda kunawatu waliokwama chini ya kifusi, huku pia kukishuhudiwa visa vya uporaji mara baada ya ajali hiyo. Polisi wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya watu waliokuwa wamekusanyika eneo la tukio.

Takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2009 na 2019,Kenya ilishuhudia majengo 86 kuporomoka na kusababisha vifo vya takriban watu 200.

Ajali hiyo imeibua upya wasiwasi kuhusu viwango vya usalama katika sekta ya ujenzi nchini Kenya.