*Lengo ni kuhakikisha Kanuni za Madini za Mazingira za Mwaka 2010 zinafuatwa

*Kuhakikisha Sheria ya Madini, Sura ya 123 na Kanuni za Haki Madini za Mwaka 2018 zinafuatwa

Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini imebainisha mikakati na mifumo thabiti inayotumika katika kusimamia wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa madini nchini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaleta tija kwa taifa huku zikizingatia usalama wa wafanyakazi na utunzaji endelevu wa mazingira.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 30, 2026 Bungeni na Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Kahama Mjini Mhe.Benjamini Ngayiwa lililouliza kuhusu mikakati ya Serikali katika kusimamia wamiliki wa leseni za uchimbaji madini ya dhahabu ili kuleta nafuu kwa wachimbaji wadogo.

Dkt.Kiruswa ameeleza kuwa , usimamizi huo unajikita katika misingi mikuu ya kisheria na kanuni zilizopo ili kuhakikisha hakuna mwekezaji au mchimbaji anayekiuka taratibu zilizowekwa.

Akifafanua kuhusu Sheria ya Madini, Sura ya 123 na Kanuni za Haki Madini za Mwaka 2018, Dkt.Kiruswa amefafanua kuwa, Sheria hii inamtaka kila mmiliki wa leseni kutekeleza kikamilifu masharti yote ya leseni aliyopewa, ikiwa ni pamoja na kuanza uzalishaji kwa wakati, kulipa mrabaha (royalties), kodi, na ada za serikali kwa wakati, pamoja na kutoa taarifa sahihi za uzalishaji.

Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, Kanuni za Ulinzi wa Mazingira kwa Uchimbaji Mdogo za Mwaka 2010, kupitia kanuni hizi, Serikali inasimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango wa Ulinzi wa Mazingira (Environmental Protection Plan – EPP).

Mpango huu unawalazimu wachimbaji wadogo kurejesha mazingira katika hali ya usalama baada ya kumaliza shughuli zao ili kuzuia uharibifu wa ikolojia na vyanzo vya maji.

Kwa upande wa Kanuni za Madini kuhusu Usalama, Afya Kazini na Ulinzi wa Mazingira za Mwaka 2010 , Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, Kanuni hizi zinamlazimu kila mmiliki wa leseni kuweka mifumo thabiti ya kulinda afya za wafanyakazi migodini, kuzuia ajali, na kuhakikisha mazingira ya kazi yanazingatia vigezo vyote vya kiusalama kimataifa.

Pamoja na mambo mengine serikali imesisitiza kuwa, kupitia Tume ya Madini na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), ukaguzi wa mara kwa mara utaendelea kufanyika migodini ili kuwawajibisha wale wote watakaoshindwa kutekeleza masharti ya leseni zao.