Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshiriki hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (27th Inter-Islands Tourism Policy Forum – ITOP 2026), ambapo amekabidhiwa bendera ya ITOP ikiwa ni ishara rasmib ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa Jukwaa la 28 la ITOP mwaka 2027.
Hafla hiyo imefanyika leo, tarehe 29 Oktoba 2026, Jeju Stone Park, Kisiwa cha Jeju, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini), na kuhudhuriwa na viongozi, wawakilishi na wadau wa utalii kutoka maeneo wanachama wa ITOP.
Bendera hiyo imekabidhiwa kwa Rais Dkt. Mwinyi na Gavana wa Jeju, Mhe. Wi Seong-gon, ikiwa ni sehemu ya makabidhiano ya uenyeji kutoka Jeju, mwenyeji wa Jukwaa la 27, kwenda Zanzibar ambayo itaandaa Jukwaa la 28 la ITOP mwaka 2027.
Makabidhiano hayo yanaipa Zanzibar nafasi ya kuwakutanisha viongozi, wataalamu na wadau wa utalii kutoka maeneo mbalimbali ya visiwa duniani, pamoja na kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni, uwekezaji na fursa mbalimbali zilizopo nchini.
Baada ya hafla ya ufunguzi, washiriki wameshuhudia maonesho ya World Island Festival, yaliyohusisha ngoma na muziki wa asili, mavazi ya kitamaduni, maonesho ya utalii pamoja na mapishi ya vyakula vya asili kutoka maeneo wanachama wa ITOP.
Maonesho hayo yametoa nafasi kwa kila mwanachama kuonesha utamaduni na utambulisho wake kupitia mavazi, ngoma, muziki, vyakula na shughuli mbalimbali za kiutamaduni, huku Zanzibar ikiwa miongoni mwa washiriki walioonesha utamaduni na vyakula vyake vya asili.
ITOP ina maeneo 12 wanachama ambayo ni Jeju, Bali, Hainan, Okinawa, Southern Province ya Sri Lanka, Hawai‘i, Zanzibar, Phuket, Cebu, Penang, Galápagos na South Aegean.
Jukwaa la 27 la ITOP linafanyika Jeju kuanzia tarehe 28 hadi 30 Oktoba 2026, likiwakutanisha viongozi na wataalamu kujadili maendeleo endelevu ya utalii wa visiwa, ushirikiano wa kibiashara, mazingira na changamoto zinazofanana katika maeneo ya visiwa.










