Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
HOSPITALI ya Manispaa ya Kibaha ya Lulanzi imeendesha kambi ya siku mbili ya huduma za macho, inayolenga kuwapatia wananchi uchunguzi wa awali, matibabu na miwani kwa wenye matatizo ya kuona.
Kambi hiyo ilianza Oktoba 28 na inatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 29, 2026, katika hospitali hiyo, ambapo wananchi wanapata huduma mbalimbali zinazolenga kuboresha afya ya macho na kuwasaidia wanaokabiliwa na changamoto za kuona.
Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa awali wa macho, matibabu kulingana na ushauri wa daktari, upimaji wa presha ya macho pamoja na elimu na ushauri kuhusu namna ya kutunza afya ya macho.
Katika siku ya kwanza ya kambi hiyo, jumla ya wananchi 110 walipata huduma, wakiwemo wanawake 87 na wanaume 23, hatua inayoonesha mwitikio wa wananchi katika kutumia huduma za afya ya macho.
Kati ya wananchi hao, 34 walipatiwa miwani huku 62 wakipatiwa dawa kulingana na mahitaji yao ya matibabu.
Kambi hiyo ni fursa kwa wananchi kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya macho kwa urahisi, huku wanaohitaji huduma zaidi wakipata ushauri wa kitaalamu kulingana na hali zao.





