Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na asasi za kiraia pamoja na taasisi za kidini katika kulinda amani, umoja, mshikaman na kuchochea maendeleo ya taifa.
Pia imeahidi kuendelea kusikiliza changamoto inazozikabili jumuiya hizo na kuzitafutia ufumbuzi kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.
Msisitizo huo umetolewa katika maadhimisho ya miaka 70 ya usajili wa jumuiya za kiraia chini yaliyo wakutanisha viongozi wa serikali viongozi wa dini na wawakilishi wa jumuiya mbalimbali kwa lengo kutathimini mafanikio yaliyopatina kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji wa taasisi hizo.
.
Katika hotuba yake Rais , Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Rais amesema jumuiya za kiraia ni msingi muhimu wa umoja, mshikamano na maendeleo ya taifa.
Amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mchango wa jumuiya hizo katika ustawi wa wananchi na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Amesema umoja wa kitaifa hauwezi kujengwa na serikali pekee, bali huanzia katika familia, shule, sehemu za kazi, maeneo ya ibada na jamii kwa ujumla.

Amesema Watanzania wanaweza kuwa na tofauti za kidini, kiitikadi,kiuchumi na kijamii, lakini tofauti hizo hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko, bali ziende sambamba na kuheshimiana,kuvumiliana na kulinda amani
Alizitaka jumuiya za kiraia kutumia nafasi zao kuchangia maendeleo ya Wananchi, hususan katika sekta za elimu, afya, upatikanaji wa majisafi na salama, ulinzi wa haki na utatuzi wa changamoto za kijamii.
Aidha, alihimiza taasisi hizo kushirikiana na serikali na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kujikita katika maslahi ya vikundi au watu
binafsi.
Katika hotuba hiyo, Rais pia alisisitiza umuhimu wa kulinda maadili utamaduni na uzalendo kwa kuwataka viongozi wa dini na jumuiya mbalimbali kuwa mfano katika kuimarisha maelewano na kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa wananchi.
Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji wa jumuiya za kiraia ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Msajili wa Jumuiya za Kiraia na dini kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Emmanuel Kihampa ametoa historia ya usajili na usimamizi wa jumuiya nchini, akibainisha kuwa mfumo huo umepitia mabadiliko makubwa
tangu kipindi cha ukoloni.
Amesema wakati wa ukoloni, sheria zilizokuwa zikitumika ziliipa serikali ya wakati huo mamlaka makubwa ya kusimamia jumuiya, ikiwa ni pamoja na kuzikagua na kufuta usajili wake.
Alieleza kuwa usimamizi huo ulikuwa na malengo ya kulinda utawala wa kikoloni, tofauti na mfumo wa sasa unao lenga kuhakikisha jumuiya zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuchangia ustawi wa wananchi.
Kihampa amefafanua kuwa kadiri mfumo wa kisheria ulivyobadilika, baadhi ya taasisi zilihamishiwa katika mamlaka nyingine za usajili na usimamizi kulingana na majukumu yake.
‘’Hali hiyo imeifanya iwe muhimu kuweka wazi tofauti kati ya aina mbalimbali za taasisi ili kila moja isajiliwe na kusimamiwa na mamlaka inayohusika ’’amesema.
Amesema jukumu la ofisi yake si kusajili jumuiya pekee, bali pia kuhakikisha taasisi hizo zinafanya shughuli zilizoainishwa katika katiba zao na kuzingatia sheria zinazotumika nchini.
Aliongeza kuwa baadhi ya taasisi zisizo za kibiashara zinaweza kutumiwa
vibaya kwa shughuli haramu, hivyo ukaguzi na uthibitishaji husadia kuzuia vitendo hivyo na kulinda usalama wa wananchi.
Amesema serikali imeweka kipaumbele katika kutoa elimu, mafunzo na ushaurii kwa viongozi wa jumuiya kuhusu utawala bora, uwajibikaji,ufanisi na namna ya kukabiliana na changamoto za kiutendaji.
‘’Lengo ni kusaidia taasisi hizo kutimiza malengo yake na kutoa huduma bora kwa jamii, badala ya kusubiri makosa yatokee ndipo hatua zichukuliwe.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema serikali iko tayari kuendelea kuwasikiliza na kuwahudumia viongozi wa jumuiya za kiraia na za kidini, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.
Amesema changamoto ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu, lakini zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za amani, maridhiano na usuluhishi.

Katambi amesema viongozi wa jumuiya za kiraia na za kidini wamekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ushauri na kushiriki katika maendeleo ya taifa
Katambi aliwahimiza kuendelea kushindikana na serikali katika kulinda umoja, haki, usawa na mshikamano wa Watanzania.
Alisisitiza kuwa serikali ina wajibu wa kutekeleza haki za jumuiya zilizo sajiliwa kisheria, huku jumuiya hizo zikiwa na wajibu wakutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kuheshimu haki za
wengine.
Alibainisha kuwa haki ya mtu mmoja inapaswa kuheshimiwa bila kuathiri haki za mtu mwingine, na kila upande unapaswa kutimiza wajibu wake ili kujenga mazingira bora ya kuishi pamoja.
Katambi pia alirejea umuhimu wa kuzingatia Katiba, sheria na misingi ya maadili inayosisitiza kuheshimiana na kutowadhuru wengine.
Aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta mbalimbali, akieleza kuwa ushirikiano na mshikamano ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo yaliyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhandisi Maryprisca Mahundi alipongeza jumuiya za kiraia kwa mchango wake katika ustawi wa jamii, hususan katika kuimarisha malezi, maadili na mshikamano wa wananchi.
Amesema viongozi wa dini na jumuiya nyingine wamekuwa wadau muhimu katika kuelimisha jamii, kukemea mmomonyoko wa maadili na kuhamasisha Wananchi kuishi kwa upendo, kuheshimiana na kushirikiana.
“Ushirikiano kati ya Serikali na jumuiya za kiraia ni muhimu katika kujenga familia imara, jamii yenye maadili na taifa lenye umoja na maendeleo watanzania kuendelea kuipenda nchi yao, kushirikiana katika kudumisha amani na kumuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aendelee kuiongoza nchi katika kuimarisha ustawi wa wananchi”amesema



