Kutoka Mkoa wa Katavi, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Kata ya Itenka A, mkulima wa matunda na mbogamboga, Frednandi Kazimili, ameeleza jinsi matumizi sahihi ya mbolea kutoka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) yalivyomsaidia kuongeza tija katika uzalishaji, kupanua soko la mazao yake na kukuza kipato.
Akieleza safari yake ya kilimo, Frednandi amesema alipoanza shughuli hizo, soko la mazao yake lilikuwa ndani ya kata anayoishi, hali iliyomchochea kuboresha mbinu za uzalishaji ili kuongeza thamani ya kilimo chake na kufikia masoko mapana zaidi.
Amesema matumizi sahihi ya mbolea za TFC, pamoja na jitihada zake za kuboresha uzalishaji, yamemwezesha kupanua wigo wa soko kutoka kuuza mazao ndani ya kata hadi kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi.
Ili kuongeza zaidi uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko, Frednandi amesema ameanzisha kilimo cha umwagiliaji, hatua inayotarajiwa kumwezesha kuendelea kulima katika vipindi mbalimbali vya mwaka bila kutegemea mvua pekee.
Ameeleza kuwa kupitia umwagiliaji, analenga kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya mazao yake, kuongeza uzalishaji na kuimarisha biashara yake ya matunda na mbogamboga.
Aidha, amewahimiza wakulima wenzake kuachana na mbinu zisizoendana na kilimo cha kisasa na badala yake kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo, kutumia mbolea kwa usahihi na kufuata kanuni bora za uzalishaji ili kuongeza tija.
Amesisitiza kuwa kilimo chenye tija kinaweza kuwa njia muhimu ya kuongeza kipato cha kaya na kukuza uchumi wa wakulima, huku akiwataka kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii.





