Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibiti
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Ali Kimara, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid inayolenga kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi na kuimarisha upatikanaji wa haki.
Kimara ameeleza kuwa kampeni hiyo inaakisi utambuzi wa Rais kuhusu mahitaji ya wananchi, hususan wanaokabiliwa na changamoto za kisheria bila kuwa na uwezo wa kumudu gharama za huduma hizo au kutambua sehemu sahihi ya kupata msaada.
Akizungumza wakati wa kuiaga timu inayotekeleza awamu ya pili ya kampeni hiyo wilayani Kibiti, Kimara amesisitiza kuwa shukrani kwa Rais zinapaswa kuambatana na utendaji unaoleta matokeo kwa wananchi.
Ameitaka timu hiyo kutekeleza wajibu wake kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, ikitambua kuwa kila mwananchi anayefika kuomba msaada ana matarajio ya kusikilizwa, kuelekezwa na kusaidiwa kupata haki.
Kimara amesisitiza kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yapimwe kwa namna wananchi wanavyopata msaada na hatua zinazochukuliwa kushughulikia changamoto zao, badala ya kuishia kuhesabu wananchi waliohudhuria.
Ameelekeza wananchi wasikilizwe kwa heshima, taarifa zao zihifadhiwe kwa usiri na kila shauri lipewe hatua inayostahili. Masuala yanayohitaji kushughulikiwa na taasisi nyingine yaelekezwe sehemu sahihi na kufuatiliwa ili wananchi wasiachwe bila mrejesho.
Aidha, ameitaka timu kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka urasimu, upendeleo na lugha zinazowakatisha tamaa wananchi, akisisitiza kuwa dhamira ya Rais ni kuona huduma hizo zikiwafikia walengwa na kuwasaidia kutatua changamoto zao.
Huduma hizo zimepangwa kutolewa kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 7, 2026, katika kata 10 za Wilaya ya Kibiti, ambazo ni Kibiti, Mtawanya, Mjawa, Bungu, Mchukwi, Mahege, Salale, Mwambao, Dimani na Mbuchi.
Wananchi wa maeneo hayo wanahimizwa kujitokeza katika vituo vilivyopangwa kwa mujibu wa ratiba ya kampeni ili kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria






