Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Gabriel Kiiza, amesema Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo limekuja kwa msisimko mkubwa kutokana na kushirikisha wasanii wengi zaidi, wakiwemo kutoka nje ya nchi.

Amesema tamasha hilo ni fursa muhimu ya kuendeleza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Tanzania, huku likiwapa wasanii nafasi ya kuonesha kazi zao na vipaji vinavyoweza kuwafungulia milango ya kutambulika ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Kiiza alisema kwa siku nne, kuanzia Oktoba 28 hadi 31, 2026, mashabiki watapata burudani mbalimbali zitakazochangia kukuza na kuenzi utamaduni wa Tanzania.

Alisema tofauti na misimu iliyopita, tamasha la mwaka huu limepanua ushiriki wa wasanii wa kimataifa, hatua inayotoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha uhusiano wa kitamaduni baina ya Tanzania na mataifa mengine.

“Tamasha la mwaka huu linafanyika kwa mara ya 44 na limekuwa tofauti kwa kushirikisha pia wasanii kutoka nje ya nchi. Hii ni fursa ya kipekee ya kuendeleza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Tanzania, huku tukijifunza kutoka nchi nyingine,” alisema Kiiza.

Aliongeza kuwa wasanii kutoka makabila mbalimbali watatoa burudani katika siku zote nne za tamasha hilo, akieleza matumaini yake kuwa mashabiki watafurahia maonesho hayo.

Kwa mujibu wa Kiiza, tamasha hilo linajumuisha shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya jukwaani, sanaa za ufundi, huduma za biashara, maonesho ya filamu, ziara za kutembelea vivutio vya utalii, warsha na mafunzo.

Tamasha hilo limeanza Oktoba 28, 2026, katika viwanja vya TaSUBa, Bagamoyo, mkoani Pwani, na linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31 mwaka huu.

Katika siku ya kwanza, tamasha lilianza kwa kishindo kwa kushirikisha vikundi vya ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali nchini, huku likihudhuriwa na umati wa mashabiki kutoka Bagamoyo na maeneo ya jirani.

Wasanii mbalimbali walipanda jukwaani na kutoa burudani iliyochochea shangwe kwa mashabiki, huku nyimbo na ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali zikionekana kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya tamasha hilo.

Baadhi ya vikundi vilivyotoa burudani ni Anga Zetu, Sauti za Umoja, Bagamoyo Collective, Bwagamoyo Africulture, Buyegu Theatre Group, Makirikiri wa Tanzania, Mindu Arts Group na Mapinduzi Arts Group.

Vikundi vingine ni Hiyari ya Moyo, Ijabalilo Entertainment Group, Freedom Band na Nasybite.

Katika upande wa kimataifa, tamasha hilo limepata ushiriki wa Elie Ongala Nyembo na Jeremie Tshimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waliochangia kuongeza ladha ya kimataifa katika maonesho hayo.

Ushiriki wa wasanii kutoka makabila na mataifa mbalimbali unalifanya tamasha hilo kuwa jukwaa la kuendeleza urithi wa kitamaduni, kukuza vipaji na kufungua fursa za kiuchumi kupitia sanaa na utalii.