Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wanawake ni wawezeshaji, walezi wa taaluma na wafungua milango ya fursa za uongozi kwa vijana hasa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Kuelekea ufunguzi wa Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 2 hadi 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan, anaonyesha nafasi ya wanawake jinsi wanavyofungua milango ya uongozi wa kimataifa kwa vijana kwa kuwajengea uwezo kwa kuanza kuwaamini na kuwateua kushika nafasi mbalimbali serikalini.
Pia anaonyesha nguvu ya wanawake kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa baadaye wa dunia na kwamba yeye ni daraja la vijana kuelekea uongozi wa majukwaa ya kimataifa baada ya Machi, 2026 kumteua Balozi Togolani Mavura kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN) wenye makao yake makuu jijini New York, Marekani.
Kabla ya uteuzi huo, Septemba, 2021 alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini pia Agosti, 2021 akamteua kijana mwingine Elsie Sia-Kanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Kitendo cha Rais Samia kuwateua kinawasukuma wanawake wengine wenye uzoefu kuwashauri na kuwaongoza vijana wenye ndoto za kushika nafasi za uongozi katika majukwaa ya kimataifa.

Vilevile kinawasaidia vijana kupata mitandao ya kimataifa na kuunganishwa na taasisi zenye ushawishi, kuwapa nafasi za kushiriki mikutano, majukwaa na programu za kimataifa, kuwajengea uwezo katika diplomasia, mawasiliano, majadiliano ya sera na kufanya uamuzi.
Kimsingi, wanawake sasa wanaanza kuvunja vikwazo vya kijamii, kiuchumi na kitaasisi vinavyozuia vijana kufikia nafasi za uongozi wa kimataifa kuhakikisha hawabaki kuwa ndugu watazamaji wa uamuzi unaofanywa katika majukwaa ya kimataifa bali wanakuwa ni sehemu ya watu wanaoyafanya.
WANAWAKE WATOA NENO
Kukazia hoja hiyo, mwandishi wa makala hii amefanya mahojiano maalumu kwa nyakati tofauti Oktoba 30, 2026 na watu mbalimbali kuhusu nafasi ya mwanamke kuwajengea uwezo vijana katika fursa za uongozi wa kimataifa.
Rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing wa Mwaka 1995, Balozi Getrude Mongella, anasema vijana wanahitaji malezi yaliyo sahihi kwa kujengwa na wazazi, jamii inayowazunguka, shuleni au vyuoni.
Anasema hiyo ni hatua ya kwanza na hatua ya pili ni elimu kwa sababu vijana hawawezi kufanya kazi ngazi ya kimataifa halafu wana viwango vidogo vya elimu.
“Elimu ndiyo itakayokupa sifa za kufanya kazi za kimataifa na kama ni ngazi ya sayansi au taaluma nyingine. Kingine ni uthubutu na hayo ndiyo mahitaji muhimu na hapo vijana watasonga mbele.
“Ndiyo maana tukirejea wakati ule wa mkutano wa Beijing kwa kweli siku zote nasema si wanawake vijana kuwezeshwa bali wasibanwe wakakosa fursa za kusonga mbele,” anasema.

Pia anasema wanawake hasa vijana wana uwezo na jambo walilolipigania ni kufungua milango iliyofungwa kuanzia elimu kwa sababu hawakuipata, uwezo wa kiuchumi na huduma finyu za afya ndiyo maana wakasema jamii isiweke vikwazo vya kuwazuia kutumia uwezo waliokuwa nao.
“Wanawake wanaweza wakipewa fursa lakini sasa hivi fursa ni nyingi. Nafasi ya uongozi lazima zifunguliwe kwa wanawake vijana kama ilivyo kwa wanaume.
“Iwe ngazi ya kitaifa au kimataifa na wachangamkie fursa na wakizipata za kimataifa waende kuzifanyia kazi kweli kweli na wasiitie aibu nchi yao na watu waseme kwamba hao ni viongozi sahihi,” anasema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema vijana wanajengewa uwezo kwa njia mbalimbali kwa mfano akionekana ana uwezo pia ana mwelekeo.

Kwa sasa, anasema mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) hapa nchini yameanzisha programu za kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapa miongozo inayotakiwa kufanywa.
“Kwa mfano unakuta kuna mtu anataka kuanzisha shirika au anataka kuelekea katika siasa. Wanapewa mentorship na hiyo ni njia mojawapo vijana wanaweza kufaidika,” anasema na kuongeza:
“Pia wanaweza kuwasiliana na kujifunza kupitia kwa watu waliopo au waliowahi kuwa huko kama Dk. Asha Rose-Migiro [Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN)] na unamuona kijana ana muelekeo wa kwenda unamwambia.
“Kwa mfano sisi katika kundi letu la WhatsApp la Shule ya Weruweru kuna wenzetu wako mashirika ya kimataifa na wakiona kuna nafasi za ajira wanazituma na kusema kama mtu ana hizo sifa kisha wanatoa mbinu za kuweza kufanikisha kuipata. Kuna njia mbalimbali kama hizo.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk. Rose Reuben, anasema wanawake wana mchango mkubwa kuwajengea uwezo vijana ili wafike katika ngazi za kimataifa kwa kuanzia katika familia.

“Kwa kuwa wanakuwa ndiyo kina baba, mama walezi na wana wajibu mkubwa wa kuwajenga vijana kuanzia watoto na kuwatia moyo na kuwaweka katika mazingira ya kuota ndoto za baadaye zitakazowasaidia kufanikisha mambo yao.
“Kwa sababu kama kijana atasema jambo linawezekana anaweza akawa kiongozi na akaenda nje ya mipaka yake mbali na familia kuanzia kata, wilaya, mkoa, taifa kikanda hadi kimataifa maana ataanza kujiamini na chochote atakifanya kwa malengo kwa sababu ana ndoto kubwa,” anasema.
Kijana akishakuwa na ndoto amezijenga, anasema zitakapotokea fursa za aina yoyote ataweza kuzichangamkia.
“Kwa hiyo hapo ni eneo la kwanza mwanamke anawajengea uwezo vijana kwenda ngazi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, eneo jingine mwanamke anakuwa tayari ameshajengewa uwezo naye anaweza kutoa ushauri na mafunzo kwa vijana hao kwa ajili ya kuwajengea uwezo wao katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Eneo langu kubwa kwa nafasi yangu ni kuwajengea vijana uwezo wa kujiamini, kujieleza pia tunapoona zile fursa tunawapatia. Kwa mfano nimepata fursa ya kusoma au kufanya kazi nje ya nchi siwezi kuiacha kwa sababu wanahitajika vijana wa umri wa miaka 18 hadi 30 bali nitakachokifanya ni kuwapa wenye sifa waipambanie kwa sababu wao hawana mtandao wanaozitoa,” anasema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Mawasiliano ya Umma wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk. Kanaeli Kaale, anasema nafasi ya vijana Watanzania kwa ngazi ya kimataifa iko chini.

“Hatuzungumzii ajira tu hata za kubadilisha uzoefu kwa mfano UN kuna programu za vijana kwenda lakini unakuta nchi za Magharibi, Kaskazini au Afrika Kusini ndio wengi lakini sisi tuko wachache kwa sababu hatuvichukulii maanani,” anasema.
Pia anachukua hatua kwa kuwatengenezea katiba wanafunzi wake ili wawe na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa katika serikali yao chuoni hapo.
“Kwa sababu hapa chuoni nimekuwa mratibu wa masuala ya ajira kwa miaka 10 wakati nilipokuwa nasoma shahada yangu ya kwanza. Nimewaambia waweke programu za kimataifa za vijana kwa sababu kwa sasa hivi zinawahusu zaidi NGOs na hapo ndipo hilo pengo linapatikana,” anasema na kuongeza:
“Kuna haja sasa hizo programu zianzishwe ndani ya vyuo vyote. Vijana waelewe wana nafasi gani katika nyanja za kimataifa na hiyo ndiyo itakayotusaidia sisi kusimamia utamaduni wetu, thamani yetu na utu wetu na tunajifunzaje kwa kushirikiana na mataifa mengine? Mimi ni mentor katika masuala ya kimataifa kwa sababu nina uzoefu.
“Vyuo vikuu kama hawajaweka wizara za mambo ya nje katika serikali zao za wanafunzi hawawezi kuingia kwenye programu za kimataifa kwa hiyo hawapati ufadhili wa masomo au kubadilisha uzoefu lakini kama wangeziweka maana yake kama ni insha au ugunduzi wa kitu fulani wangeshiriki.”
Anasema kuna wanafunzi wanasoma kozi za mawasiliano au uhusiano wa kimataifa lakini hawajui kama wanaweza kushiriki na kuwa miongoni mwa programu za jamii ya kimataifa.
“Wamezisoma na kuwa nazo tu lakini unapotengeneza programu au nyenzo na kumuelewesha wewe ni mmoja wa jamii ya kimataifa unamsaidia mwanafunzi.
“Lakini wakiweka hizo wizara ndipo watajigundua kumbe na wao ni sehemu ya hiyo jamii na wakishiriki makongamano na semina watapata uzoefu wa kupambana katika nafasi za kimataifa na raia wa nchi nyingine,” anasema.
Anawataka wanafunzi wajifunze lugha tofauti kwa kusema: “Nimewaambia wanafunzi wamekuja chuo kinafundisha Kifaransa na Kichina bure lakini watu hawajifunzi na madarasa yako tupu, kwa nini hawajifunzi?
“Nawashauri wajifunze na wachangamkie kujifunza lugha mbili za kimataifa, nashangaa walimu wa hizo lugha wapo lakini wanafunzi hawapo! Sasa tutaendaje kimataifa kama hata lugha mbili hawataki kusoma? Tutawezaje kuingia katika soko la kimataifa kama vijana hawataki kujifunza lugha hizo?”
Mratibu Taifa wa Kituo cha Usuluhishi (CRS), Dk. Gladness Munuo, anasema ipo mikakati kadhaa hapa nchini ya kuwapigania vijana hasa wanawake washike nafasi za uongozi katika majukwaa ya kimataifa kupitia nyanja mbalimbali za elimu, uchumi na siasa.

“Mikakati hiyo ni pamoja na kuwapa elimu vijana wanawake kwa kuwawezesha kupata mikopo midogo midogo, kutoa ufadhili wa elimu ya juu na kuwapatia vitendea kazi.
“Sera na sheria ziliboreshwa ili kuhakikisha sura na sauti za wanawake vijana zinaonekana na kusikika kila mahali. Kwa asilimia 40 mpango huo ulifanikiwa,” anasema.
Anashauri mikakati hiyo itumiwe kwa vijana ili wawanyanyue wenzao pia anawataka wawe na uvumilivu kwa ajili ya kutimiza ndoto zao.
Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana ya UN nchini Tanzania (YUNA Tanzania), Suzane Sylvester, anasema wao wana nafasi ya kuwaandaa vijana kushiriki katika mijadala ya mikutano ya kimataifa na programu za uongozi.

Anasema fursa hizo zinawajengea vijana uwezo wa kuwakilisha mawazo yao na nchi yao katika majukwaa makubwa ya kimataifa.
Anataka wanawake viongozi washirikiane kuvunja vikwazo vya kimtandao na kuhakikisha vijana wanapata watu na taasisi zinazoweza kuwaendeleza.
Hata hivyo, anakataa kuwaandaa vijana kwa muda mrefu bila kuwapa majukumu bali anataka wapewe nafasi za kuongoza, kufanya uamuzi na kuwakilisha taasisi na nchi.
Nini kifanyike? Anataka wanawake waliopo katika nafasi za uongozi wawe tayari kuwaongoza na kuwashauri vijana.
Pia anataka kuwe na mafunzo ya diplomasia, kuzungumza katika hadhara, uongozi, sera na ushawishi na majadiliano.
Anasema hataki tuishie kuwapa vijana mafunzo bali waunganishwe na ufadhili wa masomo, fursa za kukuza uwezo wa uongozi, mafunzo kwa vitendo na nafasi za kushiriki katika mikutano ya kimataifa.
“Napenda kusisitiza jambo moja kwamba hatupaswi kusubiri wanawake vijana wawe na vyeo vikubwa ndipo tuanze kuwaandaa kwa uongozi wa kimataifa. Tunapaswa kuanza mapema, kuwajengea uwezo, kuwaamini na kuwapa nafasi,” anasema.
Katika hatua nyingine, anasema anaamini wanawake wana nafasi kubwa kuwajengea uwezo vijana kupata nafasi za uongozi katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
“Pia naamini kwamba jukumu la mwanamke haliishii tu kupigania nafasi yake mwenyewe bali ni kuhakikisha anafungua milango kwa wengine. Kama wanawake, tunapaswa kuwa washauri na walezi wa kitaaluma, mfano wa kuigwa na wawezeshaji wa fursa.
“Tunapaswa kuwasaidia vijana kujenga kujiamini, uwezo wa kuzungumza na kujadiliana, uelewa wa masuala ya kimataifa, diplomasia, uandishi wa sera na uwezo wa kushiriki katika majukwaa ya kimataifa,” anasema.

