Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Ndaki ya Sayansi za Jamii, kimeandaa Mkutano wa Kimataifa wa Sauti ya Sayansi za Jamii (VSS2026), kwa lengo la kujadili nafasi, mchango na changamoto zinazowakabili vijana wa kizazi cha Gen Z katika kuamua mustakabali wa jamii za Afrika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Jamii wa UDSM, Dkt. Richard Sambaiga, amesema mkutano huo utafanyika Novemba 5 na 6, 2026, chuoni hapo, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Kutafakari Upya Leo na Kesho: Kizazi cha Gen Z na Harakati za Kijamii Barani Afrika.”
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kutoa jukwaa la kutafakari kwa kina nafasi ya vijana katika uongozi, utawala, uwajibikaji wa taasisi za umma na ushiriki wao katika mijadala ya kitaifa, pamoja na namna wanavyoweza kuchangia kujenga jamii yenye uwazi na ushirikishwaji.
Aidha, amesema mkutano huo utajadili mchango wa teknolojia za kidijitali na mitandao ya kijamii katika kuibua mijadala, kusambaza taarifa, kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kuwawezesha vijana kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.
Ameeleza kuwa masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na changamoto za ajira, fursa za kiuchumi, mazingira ya kujipatia kipato, jinsia, mahusiano ya kijamii, utambulisho, tofauti za kimapato, mabadiliko ya tabianchi, utamaduni, elimu na uzalishaji wa maarifa.
Dkt. Sambaiga amebainisha kuwa mkutano huo utawakutanisha wanataaluma, watafiti, vijana, wawakilishi wa asasi za kiraia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania, nchi nyingine za Afrika na nje ya bara hilo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mawazo yatakayosaidia kuelewa nafasi ya kizazi cha Gen Z katika kuunda mustakabali wa jamii za Afrika.
Amesisitiza kuwa mkutano huo unalenga kuhakikisha sauti, mawazo, matarajio na mahitaji ya vijana yanapewa nafasi katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii na mustakabali wa bara la Afrika.


