Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibiti

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Ali Kimara, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula wakiwa shuleni ili kuboresha lishe na kuongeza ufaulu.

Kimara amewataka Wakuu wa Idara za Elimu ya Msingi na Sekondari kuhakikisha shule zinaimarisha uzalishaji wa chakula kupitia mashamba ya shule, hatua itakayosaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi na kuhakikisha hakuna anayekosa chakula.

Akizungumza katika kikao cha robo ya kwanza cha Kamati ya Lishe ya Halmashauri kilichoshirikisha menejimenti, Oktoba 4, 2026, amesema upatikanaji wa chakula shuleni ni jambo muhimu katika kuboresha afya, lishe na uwezo wa wanafunzi kujifunza.

“Tuhakikishe wanafunzi wetu wote wanapata chakula shuleni na si baadhi yao.

” Tutumie vizuri mashamba yetu kwa kuwa yatasaidia kuongeza upatikanaji wa chakula na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu,” amesema Kimara.

Vilevile amezitaka shule kuimarisha upandaji wa miti ya matunda, ikiwemo mipapai, ili kuongeza upatikanaji wa matunda na kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo bora na wenye virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji na maendeleo yao.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya shule, wazazi na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha kutosha na chenye ubora wa lishe, hivyo kuchangia maendeleo ya elimu katika Halmashauri hiyo.