Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mvua zilizoanza kunyesha katika baadhi ya maeneo nchini zimetafsiriwa kuwa ishara ya kuanza kwa msimu wa mvua za vuli, huku hali hiyo ikiibua umuhimu wa serikali na wananchi kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
Hatua hiyo inakuja kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), uliotolewa Agosti 18, 2026, ikieleza kuwa msimu wa mvua za vuli wa Oktoba hadi Desemba mwaka huu unatarajiwa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya El – Niño yenye nguvu.
Katika utabiri huo, mamlaka ilieleza mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, amesema vipimo vya joto la bahari katika eneo la Niño 3.4 vilifikia nyuzi joto 2.2 Agosti na vilitarajiwa kuongezeka hadi nyuzi joto 3.6 ifikapo Desemba, mwaka huu.
Hali hii inaonyesha umuhimu wa kutazama utabiri wa hali ya hewa si kama taarifa za kawaida zinazotolewa na mamlaka husika, bali kama nyenzo muhimu ya kupanga shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya taifa.
Mvua zinapoanza kunyesha baadhi ya maeneo, jamii inapaswa kuelewa kuwa jambo la msingi si kusubiri mvua kubwa au mafuriko yatokee ndipo hatua zichukuliwe, bali ni kutumia taarifa za mapema kujipanga na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Ni ukweli mvua zina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya nchi, hususan sekta ya kilimo, ufugaji, uzalishaji wa nishati ya maji na upatikanaji wa rasilimali za maji. Hata hivyo, mvua zinapozidi kiwango cha kawaida, zinaweza kugeuka kuwa chanzo cha changamoto kubwa endapo maandalizi hayatakuwa ya kutosha.

Kwa mfano, maeneo yenye makazi yaliyojengwa katika mabonde, pembezoni mwa mito na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanaweza kukumbwa na mafuriko yanayoweza kusababisha vifo, uharibifu wa nyumba, mashamba na mali za wananchi.
Miundombinu ya usafiri kama barabara, madaraja, reli na bandari inaweza kuathirika kutokana na maji mengi, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa njia za mawasiliano. Hali hiyo inaweza kuvuruga shughuli za biashara, usafirishaji wa mazao na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Kutokana na hali hiyo, serikali haina budi kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo, badala ya kusubiri maafa yatokee ndipo kuanza kutafuta suluhisho.
Jambo la kwanza, ni kuhakikisha kuwa halmashauri zote, hususan katika maeneo yaliyotajwa na TMA kupata mvua za juu ya wastani, zinafanya tathmini ya maeneo hatarishi na kuweka mikakati ya kukabiliana na mafuriko.
Mifereji ya maji inapaswa kusafishwa na kurekebishwa, madaraja yenye changamoto za kiusalama kukaguliwa na maeneo yenye uwezekano wa kukumbwa na maporomoko ya ardhi kutambuliwa mapema.
Mamlaka zinazohusika na usafiri zinapaswa kufanya ukaguzi wa kina wa miundombinu yake ili kuhakikisha inakuwa katika hali inayoweza kuhimili changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua.
Ni muhimu pia serikali kupitia vyombo vyake vya maafa kuhakikisha kuna vifaa vya uokoaji, timu za kukabiliana na dharura na utaratibu wa kuwahamisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko.
Kwa upande mwingine, wananchi wanapaswa kubadilika na kuanza kuchukulia taarifa za TMA kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kusubiri madhara yatokee ndipo waanze kuchukua tahadhari. Hali hii inapaswa kubadilika kwa sababu taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinapotolewa mapema, zinatoa fursa ya kufanya maandalizi kabla ya changamoto hazijatokea.
Wananchi wanapaswa kuepuka kujenga makazi katika maeneo ya mabonde na mikondo ya maji, kutupa taka kwenye mifereji, kuvuka mito yenye maji mengi na kupuuza tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika.
Kwa wakulima, huu ni wakati muhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa kupanga shughuli zao za kilimo. Ni vema kuzingatia muda wa kupanda, aina ya mazao yanayofaa katika maeneo yao na ushauri wa maofisa ugani ili kuepuka hasara zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi au mabadiliko ya hali ya hewa.
Wakulima wanapaswa kuzingatia ushauri kuhusu uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna ili kupunguza uwezekano wa kuharibika kutokana na unyevunyevu na maji mengi.
TMA nayo ina jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa za utabiri zinafika kwa wananchi kwa wakati na kwa lugha rahisi ili kueleweka. Ni muhimu kuendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi na uwezekano wa kutokea kwa matukio hatarishi.
Taarifa hizo zinapaswa kuwafikia wananchi wa vijijini na mijini kupitia redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na viongozi wa ngazi za mitaa na vijiji.
Vyombo vya habari navyo vina wajibu wa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa, si kutoa taarifa za mvua zinapoanza kunyesha pekee, bali pia kueleza hatua ambazo wananchi wanapaswa kuchukua ili kujilinda.
Jambo jingine lisilopaswa kupuuzwa ni umuhimu wa utunzaji wa mazingira. Uharibifu wa misitu, ujenzi holela, kuziba mikondo ya maji na uharibifu wa vyanzo vya maji vinaweza kuongeza athari za mvua nyingi katika maeneo mbalimbali.
Hivyo, serikali na wananchi wanapaswa kushirikiana katika kuhifadhi mazingira, kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inazingatiwa.
Ni muhimu pia kuelewa kuwa utabiri wa mvua za juu ya wastani si lazima maana yake kila eneo litapata mvua nyingi kwa wakati mmoja au kila siku. Hali ya hewa inaweza kutofautiana kati ya eneo moja na jingine, hivyo wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za karibu zaidi zinazotolewa na mamlaka.
Kwa ujumla, kuanza kunyesha kwa mvua katika baadhi ya mikoa kunapaswa kuwa kichocheo cha kuchukua hatua, si sababu ya kusubiri madhara yatokee. Utabiri ni fursa ya kuokoa maisha, kulinda mali na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Serikali inapaswa kuweka mazingira wezeshi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza, huku wananchi wakitimiza wajibu wao kwa kufuata maelekezo ya wataalamu na kuchukua tahadhari zinazostahili.
Katika msimu wa mwaka 2024/2025, takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonesha uzalishaji wa mazao ya chakula uliongezeka hadi tani milioni 23.78, huku kiwango cha utoshelevu wa chakula kikifikia asilimia 130.
Akizungumza na Jamhuri Digital, Afisa kilimo kutoka mkoani Ruvuma, Emmanuel Lucas Mtenga, anashauri ni vyema Serikali ikashirikiana na maafisa ugani kutoka mikoa yote nchini kuwatembelea wakulima na kutoa elimu ya namna ya kilimo chenye tija katika katika kipindi hiki cha mvua za el nino ili wakulima walime mazao yenye kustahili.
“Bado wakulima wengi nchini hawajapata elimu ya kina juu ya mvua kubwa za el nino hivyo wanachosubiri mvua zianze kunyesha na wao waanze kilimo, kuna uwezekano wa kupoteza nguvu kubwa kwenye kilimo na mazao kuharibika na hata fedha zitokanazo na maandakizi ya kilimo” anasema.
Anasema kuwa kwa mujibu wa taarifa Serikali kuna kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini, ambacho kimefikia asilimia 130, hali inayoiwezesha Tanzania kukidhi mahitaji yake na kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya kikanda na kimataifa.
Hata hivyo bado elimu inatakiwa kwa wafugaji kwani katika kipindi hicho wanyama wanahitaji kupata huduma kama chakula hivyo wafugaji wakawa na njia nzuri ya kuwatunza wanyama kwa kuwapatia huduma bila ya kikwazo.

EL NIÑO YAANZA KUTAWALA
Mwezi wa Novemba 2026 baadhi ya mikoa imeanza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, mfano mkoa wa Kigoma na Mbeya.
Kwa mujibu wa mwelekeo wa mvua hizo, maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro.
Aidha, mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani katika kipindi hicho.
Hata hivyo, mvua nyingi zaidi zinatarajiwa kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu, kuanzia Novemba 2026 hadi Januari 2027, ikilinganishwa na kipindi cha Februari hadi Aprili 2027.
Kutokana na mwenendo huo wa mvua, baadhi ya maeneo yanaweza kukabiliwa na vipindi vya unyevu uliopitiliza kwenye udongo pamoja na mafuriko, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.
