📌 Ni kufuatia hitilafu katika njia ya kusafirisha umeme ya ardhini yenye msongo wa kV 132 eneo la Gongolamboto.

📌 yaeleza hatua za dharura zilizochukuliwa kuhakikisha huduma inaendelea kupatikana kwa wananchi huku wataalamu wakirekebisha hitilafu hiyo.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefafanua chanzo cha changamoto ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti iliyojitokeza siku za hivi karibuni ambayo iliyosababishwa na hitilafu katika njia ya kusafirisha umeme chini ya ardhi (underground cable) iliyoko katika eneo la Gongolamboto, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 5, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema hitilafu hiyo ilianza kujitokeza Novemba 3, 2026, katika njia ya usafirishaji umeme ya msongo wa kilovoti 132 (132kV), inayopeleka umeme kutoka Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto kwenda katika vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni.

Amesema mara baada ya kubaini hitilafu hiyo, TANESCO ilichukua hatua za haraka kwa kuwahamishia wateja katika njia mbadala ya usafirishaji umeme ili kuhakikisha huduma inaendelea kupatikana wakati wataalamu wakiendelea na matengenezo.

Hata hivyo, ameeleza kuwa njia hiyo mbadala ina uwezo mdogo wa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja, hali inayosababisha changamoto ya upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo, hususan wakati wa mchana ambapo mahitaji ya umeme huwa makubwa.

“Tunawaomba radhi wateja wetu walioathirika na changamoto hii. Tunatambua umuhimu wa huduma ya umeme katika shughuli za kila siku za wananchi na biashara zao. Wataalamu wetu wanaendelea na kazi ya kurekebisha hitilafu hiyo ili kurejesha huduma katika hali ya kawaida.,” amesema Bi. Gowelle.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia Usafirishaji Umeme, Mhandisi Zakaria Mgalama, amesema mifumo ya TANESCO imeundwa kwa namna ambayo hitilafu inapotokea katika njia moja ya usafirishaji umeme, huduma inaweza kuendelea kupitia njia nyingine mbadala, hatua inayosaidia kupunguza athari kwa wateja.

Ameeleza kuwa njia hiyo ya msongo wa kilovoti 132 husafirisha umeme kutoka Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto kwenda katika vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni, vinavyohudumia maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na baadhi ya maeneo ya mikoa jirani.

“Mafundi na wataalamu wetu wanaendelea na kazi ya kurekebisha hitilafu hiyo. Tunatarajia kuwa ndani ya siku chache zijazo changamoto hii itakuwa imetatuliwa. Tunawashukuru wananchi kwa uvumilivu na ushirikiano wao wakati tukifanya kazi ya kurejesha huduma katika hali ya kawaida,” amesema Mhandisi Mgalama.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mgalama amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme inayolenga kuongeza uwezo wa usafirishaji na kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Mkuranga, pamoja na njia ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Pugu hadi Dundani, ambayo itasaidia kuimarisha miundombinu ya usafirishaji umeme na kuboresha huduma katika maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam na maeneo mengine yatakayohudumiwa na miradi hiyo.