*Gati jipya la mita 300, kina cha mita 13, laleta mapinduzi makubwa

*Mzigo wapanda kutoka tani 400,000 hadi tani milioni 2.6 ndani ya miaka mitano

*Malawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Msumbiji zaitumia

*Bandari ya makaa ya mawe Kisiwa Mgao, saruji inajengwa kwa bilioni 434

*RC Mtwara akaribisha wawekezaji, asema fursa nyingi za biashara zinapatikana

Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Mtwara

Fumba na fumbua macho na kama umewahi kufika Mtwara rejea kumbukumbu ya picha ya zamani. Pia kama haujawahi kufika fanya rejea ya kumbukumbu ya simulizi za Mtwara ulizowahi kuzisikia kwa njia mbalimbali.

Kama kumbukumbu hizo bado unazo kichwani mwako anza kuzifuta kuanzia sasa kwa sababu Mtwara ya zamani uliyoisikia au kuiona imebadilika. Mtwara ya sasa ni tofauti. Shughuli za kiuchumi, biashara na uzalishaji zimeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Kwa nini kuna ongezeko hilo? Jibu la swali hilo ni rahisi kabisa kwamba kuna maboresho makubwa ya kiutendaji, miundombinu na vifaa vya kisasa katika Bandari ya Mtwara yamefanyika. Kwamba maboresho hayo ndiyo yamesababisha hayo yanayoelezwa katika habari hii? Jibu ni ndiyo kwa sababu namba hazidanganyi.

Historia na mapinduzi ya miundombinu

Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI ofisini kwake hivi karibuni, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema bandari hiyo ya kimkakati inasimamia shughuli za bandari ndogo za Kilwa Kivinje, Kilwa Masoko na Lindi zilizoko mkoani Lindi na bandari hiyo ni moyo wa uchumi wa nchi.

“Bandari hii ilijengwa miaka ya 1950 ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka kwenye gati lenye urefu wa mita 385 na kina cha mita 9.5,” anasema.

Anasema kuna maboresho yamefanyika bandarini hapo ikiwamo ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na kina cha mita 13.

Mradi wa maboresho anasema umekamilika Desemba 31, 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 157.8 na kutekelezwa na Kampuni ya CRMBEG na kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kufikia tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka kutoka tani 400,000 kwa mwaka.

Eneo lote la Bandari ya Mtwara, anasema lina jumla ya hekta 2,719 likijumuisha hekta 70 ilipo bandari ya sasa, hekta 25 kwenye vijiji vya Kisiwa na Mgao kunakoendelezwa bandari mpya ya kimkakati ya kuhudumia mzigo kwa wingi (bulk cargo) na eneo la hekta 2,624 zilizoko vijiji vya Ng’wale na Msangamkuu ambako kumetengwa kwa ajili ya mipango ya muda mrefu ya upanuzi wa shughuli za bandari.

Anasema bandari hiyo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji biashara kwenye ushoroba wa kusini, sasa inahudumia mizigo ya kimataifa (transit) kwenda nchi za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Msumbiji.

“Wakati huo kabla ya maboresho tulihudumia zaidi mazao na korosho ndilo zao letu kubwa. Kipindi chote hicho hatukuwahi kufikia zaidi ya tani 400,000. Maboresho makubwa yamefanywa kwa kujenga gati kubwa. Tulipata gati nyingine kubwa tunayoiita mpya.

“Gati namba nne kwa sababu ile ya zamani ina namba moja, mbili na tatu. Hii mpya ni kubwa na ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na ilianza rasmi Desemba 30, 2020. Tangu kipindi hicho tumeona mabadiliko makubwa katika utendaji wa bandari,” anasema.

Tangu wameanza kutumia gati mbili (ya zamani na mpya) kwa wakati mmoja, anasema mizigo inaongezeka mwaka hadi mwaka.

“Kama umeona huko nyuma hatukuwahi kufikia mzigo wa tani 400,000 kwa mwaka. Baada ya gati mpya mzigo ukaongezeka hadi kufikia tani milioni mbili na mwaka hadi mwaka tunaongeza tani zetu kwa maana mizigo tunayosafirisha kupitia bandari hii.

“Ile gati ya zamani ina mita 385 lakini kina chake ni mita 9.5 sasa na kwa sababu imeendelea kutumika muda mrefu uko mpango wa kuongeza kina ili gati ya zamani iweze kuhudumia meli kubwa zaidi,” anasema.

Kwa sasa anasema uwezo wa bandari ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 245 huku wakiwa na maegesho ya urefu wa mita 385 na mita 300 za gati jipya na kufanya jumla maegesho yenye urefu wa mita 685.

Mizigo na masoko ya kimataifa

Rekodi ya mwisho kabla ya maboresho, anasema walihudumia tani 312,000 za mzigo na baada ya maboresho wamefika tani milioni 2.6, sasa hivi wanaikimbiza tani milioni tatu.

“Nitoe picha halisi, sisi tunasimamia pia Kilwa na Lindi na miundombinu na shughuli za kiutendaji zinawajibika hapa. Bandari inahudumia mizigo mbalimbali ikiwamo makaa ya mawe, saruji, mizigo mchanganyiko inayojumuisha magari makubwa na mitambo, mazao ya kilimo ikiwamo korosho, ufuta na mizigo ya kimkakati ya miradi mikubwa,” anasema.

Kwa korosho kwa wingi anataja mchanganuo wa mzigo wake kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwamba ulisafirishwa tani 219,087, mwaka 2024/2025 tani 366,333 huku kwa mwaka 2025/2026 tani 237,094.

Huku makasha (korosho) anataja mchanganuo wake kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ulisafirishwa tani 189,841, mwaka 2024/2025 tani 90,273 na mwaka 2025/2026 tani 257,199.

Meli kubwa zikisubiri mizigo kushushwa Bandari ya Mtwara. (2)

Kwa upande wa saruji anataja mchanganuo wake kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ilisafirishwa tani 194,479, mwaka 2024/2025 tani 234,793 na mwaka 2025/2026 tani 392,304.

Makaa ya mawe anataja mchanganuo wake kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 zilisafirishwa tani 1,074,931, mwaka 2024/2025 tani 1,815,944 na mwaka 2025/2026 tani 865,133.

Mchanganuo wa mafuta kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 anataja walipakua tani 40,958, mwaka 2024/2025 tani 44,497 na mwaka 2025/2026 tani 271,745.

Anataja mchanganuo wa mzigo wa bidhaa nyingine kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ulisafirishwa tani 7,965, mwaka 2024/2025 tani 25,492 na mwaka 2025/2026 ni tani 199,777.

Kwa ujumla anasema mwaka wa fedha wa 2023/2024 wamehudumia tani 1,727,261, mwaka 2024/2025 tani 2,577,332 na mwaka 2025/2026 tani 2,223,248.  

“Katika kipindi cha mwaka 2025/2026 na mwaka 2024/2025 utaona kuna upungufu kwa asilimia 13.7. Kupungua kwa shehena kulisababishwa na kupungua kwa usafirishaji makaa ya mawe kwa tani,” anasema.

Hata hivyo, anasema sasa mzigo wao mkubwa wanaosafirisha ni makaa ya mawe.

“Baada ya uchimbaji katika maeneo ya ushoroba hasa Ruvuma, makaa ya mawe yameongezeka na tulipata bahati kwa kupata wateja walioona watumie bandari yetu. Tumepata mafanikio makubwa tangu tuanze kusafirisha makaa ya mawe.

“Tunasafirisha bidhaa za kilimo na kwa ukubwa ni korosho, sasa tunakwenda katika msimu. Mbaazi zinakwenda India, korosho zinakwenda India na Vietnam. Makaa ya mawe yanakwenda UAE, India, Pakistan na nchi za Ulaya, Kenya na DRC,” anasema.

Anasema wanahudumia mafuta (petroli na dizeli) kwa kiwango kikubwa.

“Tunafanya huduma za transit ya mafuta kwenda Zambia, Malawi, DRC, Rwanda na Uganda na Burundi. Hiyo ni sehemu tunaweza kujivunia kwamba ni mafanikio tuliyoyapata. Tuna wateja wanaopitisha mitambo na magari makubwa.

“Kuna malori makubwa yanashuka bandarini kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi mbalimbali. Pia mizigo mbalimbali ya miradi ya kimkakati inayofanywa na serikali na sekta binafsi nayo inapita hapa bandarini,” anasema.

Desemba, 2025 anasema walianza kuhudumia magari kwa kupata meli ya kwanza.

“Ni mzigo ulioanza kushushwa wakati huo sasa hivi tunaufanyia tathmini kuona tutaboresha kiasi gani? Tangu tumeanza tumeshusha magari 3,000 katika bandari yetu.

“Huduma ya kusafirisha petroli na dizeli baada ya kushushwa katika bandari yetu ni ya muda mrefu lakini miaka ya nyuma tumekuwa tunapokea meli ndogo za tani 2,000 hadi 3,000 kwa ajili ya soko la ndani lakini shughuli za uchumi zimepanuka na uhitaji kwa nchi zinazotunguzuka umeongezeka ndiyo maana huduma za bandari zimeongezeka lakini hii imechangiwa na maboresho ya miundombinu ya upokeaji mafuta tuliyofanya,” anasema.

Kuhusu upakuaji mafuta, anasema wameongeza uwezo wa paipu zao za kupokea kutoka inchi nane hadi inchi 12.

“Hata wapokeaji wetu wamefanya maboresho ya miundombinu yao na kuongeza ukubwa wa paipu za kupokea mafuta kutoka inchi nane hadi 12. Ufanisi wetu umeongezeka mara mbili tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema.

Ufanisi anasema umeongezeka mara mbili kutoka tani 800 hadi 2,000 kwa saa moja baada ya maboresho ya miundombinu ya kuhudumia makasha.

Wakati msimu wa korosho unaanza Oktoba, 2026, anasema makasha (makasha) wanayapata kutoka kwa wadau wao ambao ni kampuni za CMA CGM, MSC, PIL, MAERSK na nyingine nyingi.

Kwa upande wa saruji anasema huduma za makasha wanapewa na Kampuni ya Inchcape Shipping Services (T) Ltd.

“Wadau mbalimbali wanashiriki kusaidia shughuli za bandari zinazoendelea sasa,” anasema.

Kuhusu mzigo wa ziada, anasema wanaendelea kuihudumia kwa sababu sasa wana uwezo wa kushughulikia hadi tani milioni nne na hapo wanaweza kusema kwamba wamezidiwa.

“Mizigo inaongezeka na mahitaji nayo yanaongezeka, kwa sababu tunashirikiana na sekta binafsi kutoa huduma na kuna wadau wamefanya uboreshaji katika miundombinu ya kuhudumia shehena inayotoka bandarini.

“Kwa hiyo inasaidia kupunguza ugumu kwa bandari lakini bado tunaujua uhimilivu wa kuzidi kuongeza mzigo,” anasema.

Miundombinu na vifaa vya kisasa

Anasema ukubwa wa yadi yao ni mita 113,807 za mraba yenye uwezo wa kuhifadhi makasha 12,950. Anasema kuna maghala mawili yenye mita 25,000 za ujazo na uwezo wa kuhifadhi tani 36,000 kwa wakati mmoja.

Vilevile anasema mitambo miwili mikubwa ya kuhudumia shehena ya makasha (STS) yenye uwezo wa kuhudumia makasha 60 kwa saa, tagi za kisasa na kreni kubwa zenye uwezo wa kuhudumia kati ya tani 30 hadi 100.

Anasema wanajivunia mitambo hiyo na serikali ilifanya uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 100 kwa miundombinu hiyo na imeleta mabadiliko makubwa katika shughuli ya kuhudumia makasha.

“Hapo awali tulikuwa na mtambo mmoja wa kuhudumia na kutupa matokeo makubwa takribani makasha 300 kwa siku lakini mwaka jana mwishoni tulifanya kamisheni ya mtambo wa pili kwa shughuli ya kuhudumia makasha na zote zinafanya kazi kwa wakati mmoja.

“Ili zifanye kazi kwa wakati mmoja ilibidi tufanye mradi mdogo wa kufua umeme na ulivyokamilika uliongeza uwezo wetu wa kuhudumia makasha kutoka 300 kwa siku hadi 550 kwa siku,” anasema.

Mradi huo anasema ulikuwa wa kuweka transfoma mpya kwa ajili ya kuongeza umeme mkubwa wa kuendesha hizo mashine.

“Mashine ya kwanza ilifungwa mwaka 2021/2022. Pia kuna mitambo mingi imeongezeka. Kuna mashine tatu zinazotoa huduma kwa wateja hasa wa saruji na mizigo inayokuja inayohitaji mashine hizo. Ufanisi wetu ni uwapo wa mitambo inayoweza kutoa huduma kutokana na matarajio ya wateja.

“Tuna mashine nyingine mbili ndogo zinazobeba tani 30 hadi 50 na zinasaidia kuhudumia mizigo ya wateja,” anasema.

Anasema kuna mtambo maalumu wa kupimia mafuta (flowmeter) na midaki ya kukagulia mizigo iliyofungashwa kwenye makasha.

Mitambo mipya baada ya kufungwa Bandari ya Mtwara

Katika hatua nyingine, anasema wameanza kufanya CFS (vituo ambavyo mizigo ya makasha hupokelewa, hupangwa, huhifadhiwa au kutolewa ndani ya bandari).

“Hayo ni maeneo maalumu ya kufanya shughuli za kuhudumia shehena mbalimbali na kuzipakia katika makasha na zimetusaidia zaidi mwaka jana kupunguza zile changamoto zinazotokea kipindi cha msimu wa korosho.

“Kwa sababu mizigo inakuja bandarini ikiwa imeshafungwa na sisi hapa tunafanya scanning ya mizigo na kuipanga katika maeneo yake kabla haijapakiwa melini,” anasema.

Mizigo inayoingia na kutoka, anasema inakaguliwa kwa kutumia skana ya kisasa iliyofungwa bandarini na inatoa picha na inatambuliwa na matokeo yanatumwa huku wakishirikiana na idara mbalimbali.

“Idara kubwa ni Forodha na inafanya tathmini ya kikodi baada ya kupata matokeo ya uchambuzi wa picha ya mzigo.

Utendaji na mwenendo wa mapato

Pamoja na mambo mengine, anasema bandari hiyo ilihudumia meli 241 ikilinganishwa na meli 208 zilizohudumiwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 16.

Anasema GRT (meli kubwa) zilipungua kutoka milioni 3.429 mwaka 2024/2025 hadi milioni 2.634 mwaka 2025/2026 kutokana na kupungua kwa meli za shehena ya makaa ya mawe kwa kipindi hicho.

Aidha, anasema idadi ya makasha yaliyohudumiwa ni 34,544 ikilinganishwa na 43,364 yaliyohudumiwa mwaka 2024/2025 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 20.3 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita.

Kuhusu mapato yasiyokaguliwa, anasema yalikuwa ni Sh bilioni 73 ukilinganisha na Sh bilioni 79 yaliyopatikana mwaka 2024/2025 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 7.5 ukilinganisha na mwaka uliotangulia.

Kwa mwaka 2026/2027, anasema wastani wa mapato kwa Julai na Agosti, 2026 ni Sh bilioni 10 ukilinganisha na wastani wa Sh bilioni sita kwa mwezi uliopatikana mwaka 2025/2026. “Mapato kwa hili nitoe shukrani kwa wadau wetu kwa sababu tuna wajibu wa kukusanya kodi na mapato yote ya huduma tunayotoa. Tunakwenda katika mtiririko mzuri.

“Mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao tuna wastani wa kukusanya Sh bilioni 10 kwa mwezi kutoka Sh bilioni sita. Kabla ya mwaka 2020 tulikusanya Sh bilioni 14 hadi 15 kwa mwaka, ilikuwa ni fedha ndogo,” anasema.

Makaa ya mawe anasema ndiyo yana sehemu kubwa kwa kuingiza mapato kutokana na mzigo unaopita bandarini hapo.

Saruji nayo anasema ina uendelevu kuisafirisha hata kabla ya maboresho waliyofanya na inawaingizia mapato.

“Tunaisafirisha kwa muda mrefu tangu uwapo wa Kiwanda cha Dangote. Korosho itakuja Oktoba lakini Machi itakata. Makaa ya mawe bei ikicheza soko la dunia ina maana usafirishwaji wake nao utapungua.

“Sisi tunatambua umuhimu wa kila mteja anayetumia bandari yetu bila kuangalia jina lake. Tunawashukuru wateja wetu wote,” anasema.

Mafanikio katika usafirishaji korosho

Hadi kufikia Machi, 2026, anasema jumla ya tani 404,797 za shehena ya korosho zilihudumiwa ikilinganishwa na tani 370,896 zilizohudumiwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia tisa.

Pia jumla ya meli 37 zenye ukubwa wa GRT zilihudumiwa kwa mwaka 2025/2026 ikilinganishwa na meli 36 zilizohudumiwa katika msimu wa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 2.8.

Kwa upande wa makasha, anasema katika msimu wa mwaka 2025/2026 jumla ya makasha 29,626 yamehudumiwa ikilinganishwa na makasha 23,436 katika msimu wa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 27.

Changamoto na hatua za kukabiliana nazo

Kuhusu upungufu wa nyavu na slings (cargo gears), anasema wamepanga kununua nyavu 200 kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa usafirishaji korosho kwa mwaka 2026/2027.

Hadi sasa anasema idadi ya nyavu zilizopo ni 80 huku nyingine 120 zikitarajiwa kununuliwa kabla ya Oktoba 10, 2026.

Aidha, anasema slings na waya ngumu zimeshanunuliwa huku idadi nyingine ya vitendea kazi hivyo ikitarajiwa kununuliwa kabla ya Oktoba 10, 2026.

Anasema walipata changamoto ya uhaba wa mitambo ya forklifts kwa kuwa nyingi zilikuwa kwenye matengenezo makubwa.

Hata hivyo, anasema sasa nne zimekarabatiwa na kurudi kazini huku nyingine nne zikiendelea na ukarabati na wana ushirikiano na sekta binafsi wanaotoa huduma ya forklifts.

Anasema wamepitia changamoto ya uwapo wa mitambo yake muhimu ya kuhudumia shehena ya saruji kuwa katika marekebisho ya muda mrefu.

Kwa sasa, anasema wataalamu wanaendelea na ufungaji vipuri vipya na wanatarajia ‘Gotwalld mbili kuwa katika shughuli za kuhudumia mizigo kufikia Oktoba 10, 2026.

Kuhusu uchache wa ‘tug boats’, anasema bandari sasa inatumia tug moja katika shughuli zake za kiutekelezaji huku marekebisho kwa zilizopo yanaendelea na wanakusudia kupewa moja kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Mipango ya kuongeza ufanisi bandarini

Kwa sasa anasema kuna ukarabati wa mitambo na ununuzi wa mitambo mipya.

Pia kuna ‘empty handler’ sita zitakazotumika kuhudumia makasha tupu na ununuzi wa nyavu 200 na ‘slings’ 110 za ukubwa tofauti. Aidha, anasema mitambo minne ya Reachstacker iko tayari kutoa huduma pindi msimu utakapofunguliwa.

“Mitambo mitatu ya Gotwald inatarajiwa kufanya kazi na ukarabati kwa mitambo yote hiyo kabla ya msimu kuanza unaendelea.

“Msimu huu tunatarajia kutumia STS mbili kwa wakati mmoja kuhudumia meli za makasha, hivyo ufanisi utaongezeka kufikia kuhudumia makasha 550 kwa siku kutoka 290 ya mwaka jana,” anasema.

Vilevile anasema wana ushirikiano na sekta binafsi katika kutoa huduma ya ukodishaji mitambo kwa dharura.

“Bandari tunashirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma ya dharura ya ukodishaji mitambo ili kuongeza ufanisi.

“Kwa sasa tuna kandarasi ya ukodishaji mitambo ya reachstacker na TTs hivyo kuwa na uhakika iwapo mitambo iliyopo itapata hitilafu au pale mahitaji yatakapoongezeka na kandarasi ya ukodishaji forklifts iko kwenye hatua za ununuzi,” anasema.

Anasema wana ushirikiano na sekta binafsi kuendesha mpango wa ‘stuffing’.

“Katika kuhakikisha ufanisi unaongezeka, stuffing kwa makasha ya korosho ghafi itaendeshwa kwa kushirikiana na sekta binafsi, hii ni kutokana na eneo la bandari kuendelea kuwa finyu kutokana na kuongezeka kwa watumiaji na mizigo bandarini.

“Kwa kufanya hivi, ufanisi wa bandari utaimarika na watumiaji wengine wa miundombinu ya bandari watapata huduma stahiki bila kuathiriwa na msongamano ndani ya bandari huku mpango madhubuti wa upangaji yadi ukitekelezwa,” anasema.

Kuhusu mpango wa kuhudumia meli kulingana na utayari hasa matumizi ya gati la zamani (Berth 1-3), anasema utaangalia utayari wa mwenye mzigo pamoja na ‘vessel seniority’ au udharura wa huduma inayohitajika huku kipaumbele kikiwa katika meli za mafuta pamoja na ‘project cargo’.

Kikao cha mipango kazi, anasema kitakuwa na uamuzi wa kupanga kazi kwa kuzingatia ufanisi unaohitajika.

Gati namba nne, anasema itaendelea kuhudumia kwa kipaumbele shehena ya makasha na makaa ya mawe kulingana na ratiba ya meli na utayari wa wateja huku kipaumbele kikubwa kikiwa kuhudumia makasha.

Kuimarisha usalama wa vyombo, makasha na watumiaji wa bandari, anasema ajali zinadhibitiwa na wameongeza idadi ya waongoza magari (traffic marshals), vibao elekezi, utekelezaji wa mpango bora wa upangaji yadi na mafunzo kwa waendesha mitambo.

Kuhusu ukarabati wa mizani, barabara kuelekea gati namba tatu na maboresho ya ‘ITOS’, anasema sasa bandari inaendelea na ukarabati na urekebishaji wa mizani yote.

Anasema uboreshaji wa eneo la Ex-STAMICO unaendelea ikiwa ni hatua mahsusi ya kuongeza uwezo wa bandari kuhifadhi makasha matupu pindi yanaposhuka kutoka melini.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi.

Ujenzi wa bandari ya Kisiwa Mgao

Kimsingi, anasema Kisiwa Mgao ni mradi wa ujenzi wa bandari ya kimkakati eneo la Kisiwa na Mgao unaogharimu Sh bilioni 434.5.

Anasema bandari hiyo inajengwa kwa ajili ya kusafirisha mizigo yenye vumbi kama saruji na makaa ya mawe. Ssasa ujenzi wake umefikia asilimia 52 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2027.

Anasema bandari hiyo ikikamilika inakwenda kuondoa shughuli za usafirishaji wa bidhaa za makaa ya mawe na saruji katika bandari ya sasa na kupelekwa nje ya makazi ya watu.

“Nia ni kuzuia uchafuzi wa mazingira. Tunatarajia baada ya kukamilika kwake itakuwa na uwezo wa kuhudumia mizigo tani milioni mbili ya mizigo kwa mwaka na inajengwa kwa fedha za ndani,” anasema.

Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao ukiendelea.

Kuhusu ujenzi wa barabara kuelekea Bandari ya Kisiwa Mgao, anasema upo katika bajeti za TPA na umepewa kipaumbele kuhakikisha magari yanakwenda kwa njia mbili, na njia mbili yanarudi.

“Kwa sasa uko katika makubaliano (Hati ya Makubaliano) kati ya TPA, TARURA (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) na TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania). TPA imeshatenga bajeti kuhakikisha barabara zinajengwa kwa haraka kwa kufuata taratibu na sheria zetu za ununuzi japo hadi sasa hatujajua zitakuwa za lami au zege,” anasema.

Kuhusu uongozi, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, anasema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua.

“Kwa sisi ambao tuna muda mrefu ndani ya TPA tunaona mabadiliko katika ngazi mbalimbali. Hakuna kipindi bandari imejipambanua kama katika uongozi wa Mbossa, kwa sababu ana maono makubwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali.

“Ni mtu ambaye maono yake katika bandari hayajikiti katika urasimu. Maono yake yanaangalia ni jinsi gani sekta hii inaweza kuchochea uchumi wa taifa letu. Unaweza kuona tunaamini uboreshaji wa miundombinu fulani unaweza kuchangia kuchochea shughuli za kiuchumi kiasi kikubwa,” anasema.

Vilevile anasema maono yake yamekwenda mbali zaidi kusaidia uboreshaji wa miundombinu hata ya reli bandarini na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari.

“Hayo yote ni maeneo yanayoongeza tija katika bandari zetu na si kutengeneza urasimu. Matokeo yanaonekana na tunaongelea mapato yetu ni zaidi ya Sh trilioni mbili kwa mwaka lakini hata TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanaweza kuwa na namba kamili kutokana na shughuli za forodha zinazofanyika katika bandari zetu,” anasema.

Wao kama wawezeshaji, anasema jukumu lao ni kukusanya tozo mbalimbali zitokanazo na shughuli za bandari na jukumu lao ni kuwezesha biashara ili nchi ikusanye mapato ya kodi katika maeneo mengine.

“Hilo tumefanikiwa kwa sababu tuna kiongozi [Mbossa] anatuonyesha njia hata sisi watendaji wake anatuchochea kuifuata na jinsi ya kuzungumza na wateja na kuwasaidia.

“Utendaji wa Mbossa wa vitendo na sisi tunawajibika kufanya. Niwe mkweli, naiona bandari inakwenda kuwa kitu kikubwa na tusiangalie bandari kwa upande wa Dar es Salaam,” anasema.

Kwa maono yake, anasema anaiona bandari inakwenda kubadilisha kabisa uchumi wa nchi yetu, hasa kupitia mipango mikubwa inayoendelea kutekelezwa na serikali.

“Si Mtwara peke yake. Itazame Bandari ya Tanga inavyokuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda unataka kuanza, tumeshaona refinery (kiwanda cha kusafisha mafuta) inataka kujengwa Tanga,” anasema na kuongeza:

“Upanuzi wa bandari unaendelea na tunaona ujenzi wa reli na barabara zitakazohudumia shehena zinazotoka bandarini. Angalia Mtwara serikali imeweka mpango wa ujenzi wa reli, angalia viwanda vinaibuka mwaka hadi mwaka, wawekezaji wakubwa wanajitokeza.

“Reli itaunganisha Mbamba Bay na nia kubwa ni kulifikia soko la Malawi kwa urahisi na kuufanya ushoroba wa kusini upunguze gharama za usafirishaji. Siri kubwa ya kupata mizigo ya nchi za jirani ni gharama nafuu za usafirishaji wa mizigo yao.”

Mwaka hadi mwaka, anasema kuna mabadiliko makubwa na tunazidi kuona maboresho makubwa kwa bandari za kusini, miundombinu, mipango ya serikali na sekta binafsi na kukua kwa mazao ya biashara.

“Unaweza kutafsiri kwa Pato (Pato la Taifa) ya Bandari ya Mtwara kwamba naiona miaka 10 ijayo ikifikisha hata asilimia 40 hadi 50. Tazama fedha wanazolipwa wakulima wa korosho zinafika hadi Sh trilioni moja, na hiyo inatokea karibu miaka mitatu mfululizo,” anasema na kuongeza:

“Hiyo ni mchango ndogo na unaweza kuiona lakini ukigusa uchumi wa mkulima kwa Sh trilioni moja si kitu kidogo na tuna nafasi ya kuongeza kwa mazao mengine. Shughuli za madini nazo zinaongezeka.

“Kwa hiyo ninabashiri kwamba miaka 10 hadi 20 ijayo Bandari ya Mtwara inaweza kuchangia asilimia 40 ya Pato, hapo haujaweka bandari za Dar es Salaam, Tanga na Bagamoyo tunaiona nayo inakuja na bandari zetu nyingine za maziwa.”

Fursa mpya za uwekezaji Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, anasema Mtwara ni lango kuu la uchumi kwa ukanda wa kusini kutokana na miradi mikubwa inayopatikana.

Kupitia mahojiano maalumu aliyofanya na JAMHURI hivi karibuni anasema: “Kuna Bandari ya Mtwara na tunaishukuru serikali na sasa inajenga nyingine kule Kisiwa Mgao na itahudumia bidhaa maalumu kama saruji na makaa ya mawe. Bandari ya Mtwara ni kichochea kikubwa cha ukuaji wa biashara katika ushoroba wa kusini.”

Pia anasema wana Mtwara wanaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa maelekezo yake ya kuhakikisha korosho zote za ukanda wa kusini zinasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.

“Mikoa inayolima korosho inahusisha Mtwara, Lindi na Ruvuma. Kwa kweli tunapata ajira na kuingiza fedha nyingi serikalini na hii imeleta fursa kwa wananchi wetu.

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza Mtwara kwa sababu fursa za kiuwekezaji zipo nyingi,” anasema.

Anawataka wananchi wa Mtwara hasa vijana na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za maboresho ya Bandari ya Mtwara ili waweze kujipatia vipato.

“Sisi kama mkoa tunaweka mazingira ya usalama kwa wawekezaji wanaokuja kuwekeza na kufanya miradi mbalimbali ndiyo maana Mtwara iko shwari. Tutalinda miundombinu iliyopo na uwekezaji unaofanywa na serikali na hilo ndilo jukumu letu na tunawavutia wawekezaji wengi waje Mtwara,” anasema.

Ajira na mzunguko wa biashara

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, anasema kwa sasa Mtwara kuna mabadiliko makubwa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI hivi karibuni, anasema kabla ya maboresho ya Bandari ya Mtwara, mkoa huo ulikuwa unapoa na hakuna pilikapilika za biashara na shughuli za kiuchumi.

“Mkoa ulitulia na shughuli zilikuwa chini mno hata mzunguko wa fedha kabla ya bandari haijaboreshwa ulikuwa changamoto kubwa. Wananchi walitegemea msimu wa korosho tu na ukiondoka fedha zote zinaisha na bandari yenyewe ilikuwa inasubiri, haikuwa na shughuli.

 “Lakini baada ya maboresho sasa hivi inachukua mizigo ya saruji na makaa ya mawe. Tunamshukuru Rais Samia kwa kufanya maboresho ya bandari zetu kuanzia ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na zinafanya kazi,” anasema.

Kwa wao Mtwara, anasema wamenufaika na maboresho hayo na sasa hivi kuna mizigo mingi na magari.

“Kwa sasa ukija Mtwara unakutana na malori na magari mapya yanashushwa bandarini badala ya kushuka Dar es Salaam. Hata nafasi ya kuyaweka hapa mjini ni shida. Bandarini yamejaa na huku nje nako yamejaa. Kwetu halmashauri ni fursa na wadau wengine kukusanya ushuru wa maegesho.

“Vijana wetu wamepata fursa ya kufanya kazi kule bandarini. Kuna fursa nyingi bandarini na hata vijana wa maeneo mengine kutoka mikoa mingine nao sasa hivi wanakuja kuchangamkia fursa hii,” anasema.