Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni miongoni mwa washiriki wa Jukwaa la 24 la “African Wildlife Consultative Forum” lililofunguliwa leo Novemba 16, 2026 katika Hoteli ya Gran Meliá, jijini Arusha. Jukwaa hilo limewakutanisha wadau wa uhifadhi zaidi ya mataifa 16 kutoka sehemu mbalimbali duniani, TANAPA inawakilishwa na Kamishna wa Uhifadhi, Massana Mwishawa akiambatana na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Maendeleo ya Biashara, Izumbe Msindai.

Jukwaa hilo lililofunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi aliyemwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) linalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika uhifadhi wa wanyamapori na kuwapa washiriki nafasi ya kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali hizo. Wajumbe pia wanajadili namna matumizi endelevu ya wanyamapori yanavyochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na umuhimu wa kuzishirikisha jamii katika uhifadhi.

Ufunguzi huo ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Alexander L. Lobora, Mtendaji Mkuu wa “Safari Club International (SCI) na Safari Club International Foundation (SCIF)” – Laird Hamberlin, Maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii (TTB), TAWA, TFS, Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, watafiti pamoja na wadau wa uhifadhi kutoka zaidi ya mataifa 16.