Na Mwandishi Wetu

 Umahiri wa utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) umewavutia wadhibiti wenza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati, Maji, Mawasiliano na Usafiri(PURA) kutoka nchini Gambia, ambao wameitembelea mamlaka hiyo kwa lengo la kujifunza mifumo na mbinu zinazotumiwa katika kutekeleza majukumu ya udhibiti kwa ufanisi.

Ujumbe huo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati, Maji, Mawasiliano na Usafiri (PURA) ya Gambia umeonesha nia ya kujifunza uzoefu wa EWURA katika usimamizi wa sekta zinazodhibitiwa, hususan mifumo ya utoaji leseni, ufuatiliaji wa watoa huduma na utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wajumbe wa Bodi ya PURA ya Gambia, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Profesa Mark Mwandosya, alisema mafanikio ya mamlaka hiyo yanatokana na kuzingatia misingi imara ya utendaji inayojengwa katika utaalamu, uwazi na uhuru wa kufanya maamuzi ya kiudhibiti.

Alisema EWURA katika kutekeleza majukumu yake huzingatia maslahi ya pande zote muhimu, wakiwemo watoa huduma, watumiaji wa huduma na Serikali, kwa lengo la kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanakuwa na tija na kuleta matokeo chanya katika sekta zinazodhibitiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PURA ya Gambia, Bibi Lucy Fye, alisema wamevutiwa na mifumo ya EWURA ya kushughulikia malalamiko ya wananchi, taratibu za utoaji wa leseni pamoja na namna mamlaka hiyo inavyofuatilia utendaji wa watoa huduma walio chini ya udhibiti wake.

Aliongeza kuwa wamevutiwa pia na mfumo wa utawala na uendeshaji wa EWURA pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa leseni na vibali, hatua inayorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiudhibiti.

Ziara hiyo inatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa kati ya taasisi hizo mbili za udhibiti, huku ikilenga kuimarisha ushirikiano katika kuboresha mifumo ya udhibiti na utoaji wa huduma kwa wananchi.