Mabadiliko ya hali ya usalama katika eneo la Afrika Mashariki yanazitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea kupitia na kuimarisha mikakati yao ya ulinzi ili kukabiliana ipasavyo na vitisho vipya na vinavyovuka mipaka ya nchi.
Wito huo umetolewa Novemba 19, 2026, wakati wa Mkutano wa Kamati ya Ushauri kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi uliofanyika Kampala, Uganda, ambapo washiriki wameeleza kuwa kulinda amani na usalama wa kikanda kunahitaji juhudi za pamoja, uratibu madhubuti na ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanachama.
Kamati hiyo, inayojumuisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Ulinzi na Wakuu wa Majeshi kutoka nchi wanachama, imesisitiza kuwa changamoto za kiusalama zinazovuka mipaka, ulinzi wa njia za pamoja za biashara pamoja na majanga ya kibinadamu yanahitaji mikakati inayotekelezwa kwa ushirikiano ili kudumisha amani, utulivu na kulinda maendeleo ya eneo hilo.
Tanzania inashiriki mkutano huo kupitia mwakilishi wake, Meja Generali Michael Mumanga kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha, washiriki wameeleza umuhimu wa kuzingatia mabadiliko ya mazingira ya kiusalama katika kuimarisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano, yakiwemo mafunzo ya kijeshi, Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja na ushirikiano kati ya jeshi na raia. Hatua hizo zinalenga kuimarisha utayari na uwezo wa majeshi ya nchi wanachama kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazojitokeza.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo inajadili maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa na Maafisa Waandamizi wa masuala ya ulinzi, kwa lengo la kuyafanyia maboresho kabla ya kuwasilishwa katika Baraza la Mawaziri la EAC Novemba 20, 2026, kwa ajili ya kuzingatiwa.
Kwa upande wake, Sekretarieti ya EAC imesisitiza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na nchi wanachama, hususan kupitia Maafisa Uhusiano wa Masuala ya Ulinzi, kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yatakayokubaliwa. Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofikiwa katika mikutano yanatekelezwa na kuleta matokeo yanayoonekana katika kuimarisha ulinzi na usalama wa kikanda.







