Walemavu mkoani Iringa wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwafikia na kutoa elimu ya fedha, ikiwemo utunzaji sahihi wa fedha na namna ya kutambua alama za usalama zilizopo kwenye noti, huku wakitaka elimu hiyo iwafikie walemavu wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Iringa, Bw. Shabani Shomari, leo Alhamisi, Novemba 19, 2026, wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na BoT mkoani humo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Bw. Shomari amesema elimu ya fedha ni muhimu kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa inawawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

“Tunaishukuru BoT kwa kutupatia nafasi hii ya kupata elimu ambayo walemavu wanastahili kuipata, hasa katika kipindi ambacho nchi inaelekea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Hata hivyo, tunatamani elimu hii iwafikie walemavu wengi zaidi, hasa wale wanaoishi vijijini,” alisema Bw. Shomari.

Awali, akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa huo, Bw. Ashery Mndalila, aliwataka washiriki kutumia elimu waliyoipata kuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa kuhamasisha utunzaji bora wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo na utambuzi wa alama za usalama kwenye noti.

Kwa upande wake, Afisa wa Benki Kuu, Bw. Sadi Makomba, amesema BoT itaendelea kutoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya fedha na uchumi.

Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kutekeleza programu za elimu ya fedha na uchumi kwa makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufanikisha azma ya ujumuishi wa huduma za fedha kwa asilimia 100.