Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 limeendelea kuwa miongoni mwa makundi yanayohitaji kupewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), baada ya kubainika kuchangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya, huku vijana wa kike wakihusika kwa asilimia 77.7 ya maambukizi hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Novemba 19, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema hali hiyo inadhihirisha umuhimu wa kuimarisha elimu sahihi kuhusu VVU, huduma za kinga na upimaji, ili vijana waweze kujikinga na maambukizi na kujua hali zao za kiafya.
Amesema takwimu za kidemografia kutoka katika mfumo wa DHIS-2 zinaonesha kuwa hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wamepima na kujua hali zao, asilimia 99.5 ya waliobaini kuwa na maambukizi walikuwa wakipata huduma za dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV), huku asilimia 98.2 ya wanaotumia dawa hizo wakiwa wamefubaza virusi mwilini.
Profesa Kabudi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, ambapo maambukizi mapya yamepungua kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025, sawa na upungufu wa takribani asilimia 66.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za afya, kuongeza upatikanaji wa dawa za ARV pamoja na kuelimisha jamii kuhusu njia za kujikinga na maambukizi na umuhimu wa kupima na kupata matibabu.
Aidha, amesema maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu yanatarajiwa kuanza Novemba 24, 2026 katika kanda saba za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), na kuhitimishwa Desemba Mosi katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yataenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TACAIDS mwaka 2001, huku kilele chake kikitarajiwa kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akiwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji,” inayolenga kuhamasisha upatikanaji wa huduma bora za afya, rasilimali na utashi wa kisiasa katika kuhakikisha mapambano dhidi ya VVU yanaendelea kwa ufanisi.
Amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji wa rasilimali za ndani, kushirikisha sekta binafsi na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kinga, upimaji na matibabu zinapatikana kwa wananchi bila kuathiriwa na mabadiliko ya ufadhili wa kimataifa.
Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030, huku akiwataka Watanzania kuachana na unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU ili kujenga jamii inayowakubali na kuwaunga mkono.
Maadhimisho hayo pia yanalenga kuwaenzi na kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI, kutathmini maendeleo ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo, kuhamasisha ushiriki wa jamii na kujadili mafanikio pamoja na changamoto zilizopo katika kufikia azma ya kutokomeza UKIMWI nchini.



