• DCEA yafichua mbinu mpya za uzalishaji, yaanzisha ufuatiliaji wa bangi aina ya ‘skanka’
  • Yajipanga kutoa elimu kwa wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza katika vyuo mbalimbali nchini
  • Mtandao wa dawa za kulevya wavunjwa Tanzania, Kenya; watuhumiwa saba wakamatwa

Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imeingia katika sura mpya baada ya kubainika kuwa baadhi ya wahusika wameanza kulima bangi majumbani mwao; JAMHURI linaripoti.

Mbali na hayo, imebainika kuwa wapo watu wengine wanaohamishia mashamba kwenye mapori na hifadhi ili kukwepa operesheni za serikali.

Mbinu hizo zimeibuka wakati Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikitangaza kupungua kwa upatikanaji wa heroin na cocaine mitaani, lakini ikikiri kuwa bangi bado inaongoza kwa matumizi na uzalishaji nchini.

Hali hiyo inaonyesha changamoto inayowakabili wadhibiti wa dawa za kulevya, kwani wakati mitandao mikubwa ya usafirishaji ikivunjwa, wahusika wengine wanabadilisha maeneo na namna ya kuendesha shughuli zao.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ameliambia JAMHURI kuwa mamlaka imebaini kilimo cha bangi ndani ya nyumba, sambamba na mashamba yanayofichwa maeneo ya mbali.

“Tumebaini hata visa vya bangi kulimwa ndani ya nyumba. Kwa upande wa mapori na hifadhi, tunashirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wahifadhi wengine kufuatilia kilimo hiki,” amesema.

Anasema bangi na mirungi zinaendelea kukamatwa kwa wingi katika operesheni mbalimbali, huku mamlaka ikifuatilia kwa makini bangi inayofahamika kama ‘skanka’.

Skanka (skunk cannabis) ni aina ya bangi inayojulikana kwa harufu kali na ambayo mara nyingi huzalishwa kutoka kwenye mimea iliyochaguliwa kwa lengo la kuongeza kiwango cha ‘tetrahydrocannabinol’ (THC), kemikali inayosababisha athari za kulevya.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 24- 30, 2026