NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SERIKALI imelitaka Shirika la Posta Tanzania kutumia ipasavyo vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vilivyokabidhiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ili kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika uchumi wa kidijitali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Novemba 26, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amesema mabadiliko ya teknolojia yamebadili mfumo wa uendeshaji wa mashirika ya posta duniani, kutoka katika kusafirisha barua pekee na kuwa vituo vya huduma za kidijitali, biashara mtandao, ujumuishaji wa kifedha na huduma za Serikali mtandao.
Amesema Tanzania inapaswa kutumia mtandao mpana wa Shirika la Posta, unaofika maeneo mbalimbali kuanzia vijijini hadi mijini, kuharakisha mageuzi hayo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisasa kwa urahisi.
Aidha, amesema uwekezaji katika vifaa vya TEHAMA ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kisasa na shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia, sambamba na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga Tanzania ya kidijitali.
Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema shirika hilo limejipanga kuhakikisha vifaa vilivyokabidhiwa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuleta manufaa kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Mlembwa Mnakua, amesema katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka uliopita wa fedha, mfuko huo umewezesha ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya Shirika la Posta Tanzania vyenye thamani ya Sh bilioni 2.5.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, UCSAF imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na kuanzisha vituo vipya vya kutolea huduma za posta, hatua inayolenga kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.


