Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbarali
Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imekamilisha ahadi ya kugawa shamba namba 78 kwa wakulima wadogo wilayani Mbarali Mkoani Mbeya .
Imeelezwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inajipanga na wakulima hao wadogo wanapata mashamba Wilayani Mbarali.
Hatua hiyo imetokana na agizo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ziara yake wilayani Mbarali Oktoba 17 mwaka huu la kuwandolea adha wakulima hao ya kukosa maeneo.
Serikali imeanza mchakato wa kuwapatia maeneo mbadala ya kilimo wakulima wadogo waliopisha eneo la hifadhi ya Ruaha katika vijiji vya Mnazi na Madibila, kupitia Shamba Na. 78 la Mbarali Highland Estate Limited lililotwaliwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kuwawezesha kuendelea na shughuli za kilimo.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Brigedia Jenerali Maulid Sulumbu, amesema kuwa agizo hilo lililenga kuundwa kwa kamati itakayoharakisha mchakato wa kuwatambua wakulima wadogo wenye sifa za kupatiwa maeneo ya kilimo katika shamba hilo.
Aidha amewataka wananchi wenye malalamiko, maoni au hoja kuhusu mchakato wa ugawaji wa maeneo katika shamba hilo kufika ofisini kwake na kuwasilisha hoja zao ili ziweze kufanyiwa kazi.
“Kwa hiyo wale wachache watakaobahatika kupata basi waridhie wakati huo Serikali yetu kupitia Tume ya taifa ya Umwagiliaji ikiendelea na taratibu za kutafuta maeneo mbalimbali Tanzania kwa ajili ya kuwapatia wananchi wengi maeneo ya kilimo.”Sulumbu
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Victoria Mwakalinga, amesema kuwa katika hatua ya kuwatambua wakulima wenye sifa, tayari kamati imesambaza fomu za maombi zenye vigezo maalumu vitakavyotumika kuhakiki na kubaini wakulima wadogo wanaostahili kupatiwa maeneo hayo.
Ameeleza kuwa hadi sasa kamati imepokea jumla ya fomu 1,200 ambazo zinaendelea kufanyiwa uchambuzi ili kubaini waombaji wanaokidhi vigezo vilivyowekwa, huku akibainisha kuwa waombaji watajulishwa matokeo ya mchakato huo baada ya kukamilika kwa tathmini.
Ameongeza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wakulima wanaohitaji maeneo hayo, ugawaji wa mashamba utafanyika kwa awamu ili kuhakikisha kila mkulima anayestahili anapata eneo la kilimo, huku akibainisha kuwa shamba hilo lina ukubwa wa zaidi ya ekari 4,000.
Baadhi ya wakulima wadogo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hiyo ya kupata maeneo ya kilimo, wakisema hatua hiyo itawawezesha kuendelea na shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.








