Tumemsikia aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akilalamika kuwa baada ya kung’atuka marafiki hawaonekani!

Baada ya kustaafu ndiyo ametambua kuwa kumbe baadhi ya marafiki walikuwa ni marafiki wa nafasi aliyokuwa nayo, na kamwe hawakuwa marafiki wa Kova. Anashangaa kuona hata wengine hawapokei simu zake.

Kwa waliosoma au kuusikia ujumbe wake wanamhurumia. Wanamuona amekuwa mpweke. Kwa kuwa wapo wanaomhurumia, bila shaka wapo pia wanaofurahi kusikia yanayowapata wastaafu wa aina yake.

Baada ya kumsikia Kamanda Kova nimewaza mengi. Nimewaza maisha ya wastaafu wa kada mbalimbali. 

Nikawaza namna ninavyowakumbuka walimu wangu wawili – Nyagabona aliyenifundisha a, e, i, o, u (darasa la kwanza), na Madaha.

Wanafunzi wengi wanawakumbuka walimu wao kwa misingi ya maisha waliyowapa hata kama ni kupitia bakora.

Kova ni polisi. Sote tunajua wajibu wa polisi ni kuwalinda raia na mali zao. Sasa iweje mtu anayetekeleza wajibu wake wa kuwalinda raia na mali zao achukiwe au akimbiwe na marafiki baada ya kustaafu? Hili ni swali la kuhangaika kupata majibu?

Polisi kadhaa si watenda haki. Sina hakika Kova alikuwa kundi lipi, lakini inawezekana kwa sababu ya picha hasi ya wananchi kwa polisi wale wachache ambao ni watenda haki wanaunganishwa kwenye kapu la polisi waonezi, dhulumati, watesi, na wakati mwingine waporaji. 

Nakumbuka kuna polisi alinipora buti zangu nikiwa mdogo. Tumefundishwa kusamehe, lakini si kusahau. Huyo sidhani kama ninaweza kupokea simu yake.

Kuna watumishi wa umma kadhaa wanaoishi maisha yasiyo halisi (artificial). Wapo wanaojulikana kwa ubabe na dhuluma. Hawanunui pombe. Hawanunui mboga. 

Hawa wakifika mahali, na kwa sababu ya nafasi zao, hudai huduma na huzipata kwa sababu ya hofu ya walengwa. 

Kuna mabwana na mabibi wakaguzi wa nyama wao ni kula maini na figo tu. Wanachukua kwa sababu ya madaraka yao. Mwenye kugoma ataambiwa nyama yake yote ni mbovu, hivyo itupwe. Matokeo yake wafanyabiashara wamevumilia ubabe huu kwa sababu ya madaraka yao. Hao wakistaafu hata msibani hawakaribishwi.

Kuna polisi na watumishi wa umma wengi ambao hawajui adha za foleni. Barabarani wanawasha ving’ora na mataa makali wapishwe hata kama wanakwenda au wanatoka mashambani. 

Wakifika kwenye mwendokasi magari yao wanayapitisha barabara za mabasi. Kwenye taa  hawasimami. Wakipakiwa kwenye pikipiki hawavai kofia ngumu (helmet). 

Katika mataifa ya wenzetu watumishi wa umma ndio wanaopaswa kuwa mfano wa tabia njema na utii wa sheria. 

Tanzania ni kinyume kabisa. Magari ya majeshi, magari ya majaji, magari ya mtu hata akiwa karani – alimradi yuko ofisi ya umma – ndiyo yenye ruhusa ya kuvunja sheria. 

Haya ni maisha artificial. Haya yanafanywa hadharani. Wananchi wana macho. Wanaona. Wananung’unika kimya kimya. Kina Kova wanaofaidi uhondo huu wakishastaafu ndipo wanapokutana na hukumu ya wananchi waliowanyenyekea wakiwa madarakani.

Watu wa aina hii wanaoishi maisha bandia hata siku zao baada ya kustaafu huwa za shida, maana ile ‘privilege’ na kunyenyekewa wanakuwa hawana tena. Hawa wanaishi kwa msongo. Hawa marafiki zao ni wenzao waliotesa kama wao.

Kuna kesi nyingi watu wanabambikiwa. Mtu anaingia rumande bure, lakini anatoka kwa kuwalipa polisi wasio waungwana. 

Watu wanauza ng’ombe kuwakomboa ndugu waliobambikiwa kesi. Hawa hukumu za kutopokewa simu zao au kupata mialiko watakutana nazo wakishastaafu.

Kuna mtu unaona hana hatia kabisa au ana sifa kisheria za kupata dhamana, lakini ananyimwa. Kuna mtu anaonekana hana haki, lakini mambo yanapinduliwa na kuwa yeye ndiye mwenye haki.

Kamanda Kova anajua kuna zawadi wanapokea maofisa wa aina yake si kwa sababu ya kupendwa, bali kwa sababu wanaozitoa wanafanya hivyo kama ‘hirizi’ dhidi ya mambo fulani fulani. 

Wapo wanaotoa kwa sababu ya woga tu. Watu wa aina hiyo hawawezi kuwapigia simu wastaafu anaosema Kova.

Kauli ya Kamanda Kova ifungue masikio ya wengi. Wajiulize ni wapi wanakosea hadi wachukiwe baada ya kustaafu? 

Wajiulize malipo gani wanatarajia kuyapata wakistaafu endapo wao kazi yao ni kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani kana kwamba katiba imeharamisha mfumo wa vyama vingi? 

Tumeona video namna polisi anavyoshiriki uporaji wa kura. Kova ajiulize, mtu anayepokwa ushindi kwa nguvu za polisi kwa namna hiyo atakuwa radhi kupokea simu ya huyo mtu akistaafu?

Kamanda Kova asilalamike tu kutopokewa simu, bali ajiulize zaidi nini kimewasibu Watanzania kiasi cha kushangilia polisi wakifikwa mabaya? 

Nini kinawafanya Watanzania washangilie polisi wakishambuliwa? Tujiulize sote, kuna nini? Wataalamu wa utafiti hawapaswi kukaa kimya. Huu ni utafiti mwepesi mno. Imani ya watu kwa vyombo vyao kama Jeshi la Polisi imeshuka. 

Wapo wanaopendekeza mfumo wa jeshi letu ubadilishwe kwa kuwa na mitaala mipya, hasa kwa kukazia zaidi kwenye mafunzo ya haki za binadamu ili kurejesha imani.

Kamanda Kova atambue kuwa si wastaafu wote wanaokimbiwa. Wapo wanaokimbiliwa kama peremende. 

Kamanda Kova anaweza kuwasaidia kwa nasaha wastaafu watarajiwa mambo gani watende na yapi waepuke ili yasiwakute kama yanayowakuta yeye na wengine wa aina yake. 

Kwangu mimi naona kuishi kwa kiasi na kuwatendea haki wanadamu ndiyo siri ya kutokimbiwa ukishastaafu. Tutende haki na tuache kuishi maisha artificial.

By Jamhuri