Wasudan waukataa utawala wa kijeshi

Na Nizar K Visram

Mwaka 2019 wananchi wa Sudan waliandamana kote nchini mwao wakimkataa Rais Omar Hassan Ahmad al-Bashir aliyetawala kwa muda wa miaka 30. Polisi walitumia silaha na raia wengi waliuawa. 

Mwishowe jeshi likalazimika kumuondoa Bashir na kumweka chini ya ulinzi. 

Baada ya hapo ikaundwa serikali ya mpito kwa ushirikianao wa majeshi, vyama vya siasa na asasi za kiraia. Jenerali Abdel Fattah al-Burhan akawa Mwenyekiti wa Baraza la Utawala na Abdalla Hamdok akawa Waziri Mkuu. Wakakubaliana kuendesha nchi pamoja wakati wakiandaa Katiba mpya kuelekea uchaguzi na serikali ya kidemokrasia. 

Hata hivyo, hali hiyo ilibadilika ghafla Oktoba 25, mwaka huu wakati Burhan alipotwaa madaraka kamili. Akatangaza hali ya hatari na kumuweka Hamdok chini ya ulinzi. Pia aliwakamata mawaziri, wanasiasa na wanaharakati.

Kwa mara nyingine wananchi wakaja juu, wakipinga hatua zilizochukuliwa na Burhan. Maandamano yakafanyika kote na polisi ikatumia nguvu. Matokeo yake watu wasiopungua 40 wamepoteza maisha yao.

Ndipo Novemba 21, mwaka huu Burhan akalazimika kumrejesha Hamdok katika kiti chake cha uwaziri mkuu na kuwaachilia baadhi ya viongozi aliowafunga. 

Makubaliano yakafikiwa kati ya Burhan na Hamdok kuunda serikali ya mpito hadi uchaguzi utakaofanyika mwaka 2023. 

Lakini mambo hayakuwa rahisi kama ilivyotarajiwa, kwa sababu vyama na asasi zilikataa maelewano mapya ya Burhan na Hamdok. 

Wakadai kuwa majeshi yajitoe na serikali ya mpito iwe ya kiraia, maandamano yakaendelea, kwa sababu waliona kuwa ingawa Hamdok amerejeshwa kama Waziri Mkuu bado mamlaka kamili yamo mikononi mwa Burhan na wanajeshi wenzake

Kwa mfano, ingawa Hamdok ndiye anayeteua mawaziri, lakini serikali yake itakuwa inasimamiwa na Burhan. Wananchi wakamshutumu Hamdok kuwa anatumiwa na jeshi ili ionekane kuwa kuna serikali ya kiraia. Pia wakati Burhan aliwaachia wanasiasa wachache bado kuna wengi wangali wamezuiliwa. Hamdok hana mamlaka ya kuwaachia.

Ndiyo maana mawaziri 12 walioteuliwa na Hamdok walijiuzulu wakipinga mamlaka aliyonayo Burhan. Miongoni mwa mawaziri waliojiuzulu ni Mariam al-Mahdi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje. 

Yeye amesema maelewano ya Burhan na Hamdok yamerejesha nyuma mageuzi ya kidemokrasia nchini humo kwa sababu hayaweki wazi mamlaka aliyonayo Hamdok na baraza lake la mawaziri.

Ingawa maelewano ya Burhan na Hamdok yamekataliwa na wananchi wa Sudan, nchi za Magharibi, zikiwamo Marekani na Umoja wa Ulaya, zimeyakaribisha kwa sababu eti ‘yamewatia moyo. 

Hivi ndivyo nchi hizo ‘zinavyounga mkono’ demokrasia barani Afrika. Haidhuru wananchi wanataka nini, mradi tu nchi hizo zimetiwa moyo.

Novemba 25, mwaka huu maelfu ya raia waliandamana katika miji ya Khartoum, Omdurman, Port Sudan, Kassala, Wad Madani na El Geneina, wakipinga serikali mpya ya Hamdok na wakilaani mauaji ya raia. Majeshi ya Sudan yaliwatupia waandamanaji mabomu ya machozi na kuwafyatulia risasi za moto.

Hasira za wananchi wa Sudan zimeelekezwa kwa Burhan pia kutokana na jinsi anavyoendesha siasa za mambo ya nje, hususan alivyowasiliana na Israel bila ya kushauriana na viongozi na wananchi.  

Mnamo Februari, 2020 Burhan alikutana mjini Entebbe na Benjamin Netanyahu aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel wakati huo. Burhan alielekea Entebbe kwa siri na mkutano ulifanyikia Ikulu ya Rais Yoweri Museveni bila ya hata kuwaeleza mawaziri wa Sudan. Hata waziri wake wa mambo ya nje hakujua.

Siku mbili baada ya mkutano huo ndipo wananchi wa Sudan wakagundua, nao wakauliza hivi ni nani aliyempa madaraka hayo Burhan? Katiba ya mpito ilieleza wazi kuwa uamuzi wowote kuhusu mambo ya nje ni lazima yapitishwe na baraza la mawaziri.

Cha ajabu ni kuwa hata Hamdok akasema yeye hakujua kuhusu mkutano huo na Netanyahu, hata hivyo alisema eti hakuwa na pingamizi lolote.

Cha ajabu zaidi ni kuwa wakati mawaziri wa Sudan walifichwa Marekani walijua mapema. Kwa maneno mengine wananchi wa Sudan waliona siasa yao ya mambo ya nje inaendeshwa na Marekani. 

Mike Pompeo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo alijua mapema kuliko mawaziri wa Sudan. Ndipo Pompeo akampongeza Burhan kwa ‘uongozi wake’ na kwa uamuzi wake wa kuanzisha uhusiano na Israel.

Chanzo cha mkutano wa Entebbe ni kuwa Hamdok amekuwa akiwasiliana na Marekani ili iondoe vikwazo vyake dhidi ya Sudan vilivyowekwa tangu enzi za Bashir. Marekani iliishutumu Sudan kuwa inasaidia ugaidi ndipo ikaiwekea vikwazo.

Sudan ilikuwa inakabiliwa na deni la dola bilioni 60 za Marekani, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 60, nchi ilikosa mafuta na fedha za kigeni. Hali ilizidi kuwa mbaya kutokana na vikwazo vya Marekani. 

Juu ya yote hayo, Marekani imekuwa ikidai dola bilioni mbili kama ‘fidia’ kwa ajili ya hujuma za Al Qaeda huko New York, ingawa Sudan haikuhusika na hujma hizo.  

Marekani haikuondoa vikwazo hata baada ya Bashir kupinduliwa. Ndipo watawala wapya wa Sudan wakaiomba Israel izungumze na Donald Trump aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo.

Netanyau alipozulu Washington alimdokeza Pompeo kuwa Sudan inaelekea kupiga magoti.  Wakati huo Trump alikuwa anaandaa kile alichokiita ‘mpango wa amani wa Israel na Palestina’. 

Mpango huo ulitangazwa jijini Washington na Trump mbele ya Netanyau na mabalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Oman na Bahrain. Pompeo akampigia simu Burhan na kumualika Washington. Burhan akavimba kwa furaha. 

“Israel ina historia ndefu ya kujaribu kukutanisha watawala wa Kiafrika na Marekani. Imekuwa daima ikitumia urafiki wake na utawala wa Marekani ili kusukuma mbele masilahi yake barani Afrika,” anasema Yotam Gidron ambaye ni mtafiti na mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Israel ndani ya Afrika’.

Hivyo mkutano wa Burhan na Netanyau ni matokeo ya mazungumzo ya Israel na Washington. Imeripotiwa kuwa jitihada pia zilifanywa na watawala wa Kiarabu kuwakutanisha Burhan na Netanyau ili Marekani iondoe vikwazo. Watawala hawa wamekuwa wakitoa misaada ya kijeshi, kiuchumi na kidiplomasia kwa Burhan na Makamu wake, Jenerali Mohammad Hamdan Daglo. Hii imeifanya Sudan ilegeze uhusiano wake na Iran uliokuwapo tangu wakati wa Bashir. 

Katika yote haya, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan aliachwa kando. Masuala ya mambo ya nje ya Sudan yamekuwa yakiamuliwa na Burhan na Daglo wanaofanya mazungmzo na nchi za kigeni.

Mbinu hizo za Israel kupenya Sudan zimepingwa na wananchi. Maandamano yalifanyika Khartoum kutokana na taarifa ya pamoja ya Israel, Sudan na Marekani ikisema Sudan na Israel ‘zimemaliza uhasama.’

Vyama vya siasa na asasi zilitoa risala zikisema wananchi wa Sudan wanawekwa gizani wakati watawala wanakutana na kukubaliana kisirisiri. 

Wakasema: “Wananchi wetu hawatageuza msimamo wao wa kihistoria wa kuunga mkono ukombozi wa Palestina.” 

Waandamanaji mbele ya ofisi za kiserikali walibeba mabango yakisema: “Hakuna makubaliano wala mazungumzo na wavamizi wa Palestina.” Wakachoma bendera ya Israel.

Wakati huohuo wananchi kote nchini humo wanaendelea kudai serikali ya kiraia na kuwataka wanajeshi warudi kambini. Novemba 30, mwaka huu polisi waliwashambulia maelfu ya waandamanaji wakitumia mabomu ya machozi na grenedi huku vifaru vimewekwa barabarani kuwazuia waandamanaji wasikaribie ikulu.

[email protected]

0693- 555373