KILIMANJARO

Na Nassoro Kitunda

Ajali za barabarani bado ni tatizo la muda mrefu, limegharimu maisha ya Watanzania wengi. Hali hiyo imesababisha kuwa na Wiki ya Usalama Barabarani, wadau wanakutana na kujadili namna ya kupunguza ama kuziondoa kabisa. 

Kila mwaka Tanzania inaadhimisha Wiki ya Usalama Barabarani, na mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa mkoani Arusha na mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan. 

Lakini bado tatizo la ajali limekuwa na linaendelea ingawa tunaambiwa kuwa kuna mafanikio ya kupungua lakini bado ajali zipo na zinaendelea kuwaumiza Watanzania. Kundi la waendesha bodaboda linatajwa kuwa ndilo linaloathirika zaidi na ajali lakini kwa ujumla madereva wa maroli, mabasi na magari binafsi nayo yanatajwa kusababisha ajali. 

Kwa hiyo kuna mjadala wa namna ya kukabiliana na ikiwamo kama vile kutoa elimu, kukagua magari, kutoza faini na mikakati mingine. 

Mbali na mikakati hiyo, lakini ni muhimu kutazama kwa undani wake kiini cha ajali za barabarani, wapi tunafanya makosa? Na upi uwe mwelekeo wetu kuhusu kupunguza ajali za barabarani? 

Tufikiri zaidi ya sababu za kibinadamu

Imekuwa kawaida kwa wadau wengi wa masuala ya barabarni na hata tafiti zinazofanywa kusema kuwa vyanzo vya ajali nyingi kwa asilimia zaidi ya tisini zinatokana na binadamu, masuala ya mwendo kasi, kuovateki na uendeshwaji wa magari chakavu. 

Lakini tafiti hizo hazitafiti zaidi ubinadamu huo ni upi? Na unasababishwa na nini? Kwanini sababu hizi zinatokea? Kwa sababu, inachukuliwa kuwa ni uzembe wa madereva kama binadamu na ndiyo maana tumekuwa tukitumia muda mwingi wa kutoa elimu kwa madereva kama njia ya kupunguza ajali. 

Kwanini amekuwa akifanya hivyo? Hata sheria zetu za usalama wa barabarani zimekuwa zikitazama mtu kama chanzo cha ajali na ndiye anayehukumiwa. 

Lakini tumesahau eneo ambalo pia lingetupa upande wa pili kwanini pia kuna ajali hizi za barabarani, mbali na jitihada nzuri zinazofanywa na wadau wa usalama wa barabarani. 

Hali za uchumi za madereva na mikataba yao

Mbali na elimu na kudhani kuwa tukirekebisha tabia za watu basi tunaweza kutatua tatizo, kumbe ndiyo kwanza tunaona tatizo linazidi. 

Hii inatuonyesha kuwa suala si elimu na kubadili tabia za binadamu, tunapaswa kufikiri zaidi kuhusu mifumo yetu ya kuwalipa madereva, masuala ya mikataba, posho zao. 

Uzoefu unaonyesha hivyo. Masuala ya mwendo kasi ni kutokana na posho ndogo wanazopata madereva na kutokuwa na mikataba, hivyo dereva anawahi ili awe na mzunguko wa angalau wa kupata fedha za kujikimu na familia yake. 

Mambo haya hayapewi uzito mkubwa katika tafiti zetu, wala katika mijadala ya wadau wa usalama wa barabarani, yanaonekana mambo madogo lakini kwa uhalisia ndiyo mambo yanayosababisha ajali, kwa sababu yanahusu maisha ya watu. 

Mwanamapinduzi wa Guinea Bissau na Cape Verde, Almicar Cabral anasema: “Siku zote binadamu apiganii mawazo bali anapigania uchumi wake – apate nguo, chakula, malazi na makazi.”Mambo hayo akiyakosa atafanya namna yoyote kupata.

Hatuna budi kutazama kwa undani, hali halisi ya mifumo yetu inayoratibu masuala ya vyombo vya moto barabarani, mifumo ninayoisema ni ya umiliki wa vyombo hivyo vya usafirishaji – nani anamiliki? 

Si kumiliki tu na faida inayotengenezwa kupitia vyombo hivyo vya barabarani nani anafaidika nayo? Maswali haya ndiyo kiini kikubwa cha chanzo cha ajali za barabarani. 

Madereva wanatumia nguvu na muda wao kukaa muda mrefu madarakani na kutengeneza faida kubwa, lakini mwishowe faida inakwenda kwa mmiliki wa gari au basi na dereva kuambulia posho isiyoweza kutatua shida zake za kila siku na familia yake. 

Tunadhani gari anaendesha dereva na kuweka mikakati kumbe kuna sababu sisi hatuzioni kwa macho ya kawaida, sababu za kiuhusiano wa mmiliki wa gari au bodaboda na mwendeshaji. 

Kumbe gari anaendesha mmiliki, sisi tunamwona dereva kumbe mmiliki ndiye anaendesha fikra na mienendo ya dereva. Kwa sababu anawaza hesabu ya bosi, posho ndogo, amepewa fedha kidogo ya kupeleka mizigo nje ya nchi, anawaza aende safari yake kwa muda mfupi ili afidie fedha chache alizopewa isiishie njiani na mwenye bodaboda anawaza namna gani atarudisha fedha za pikipiki ya mkataba. 

Mambo haya ndiyo yanendesha gari na si dereva kama tunavyodhani tunamuona pale katika usukani. Lakini kwa bahati mbaya mikakati yetu haiyatazami haya. Hivyo, kama tuna nia ya dhati ya kutatua tatizo hili lazima tuanzie huku katika uhusiano wa huyu dereva na mmiliki wa chombo husika. 

Tufanye nini?

Swali hili ndilo la msingi baada ya kutambua wapi  tunakosea, sasa inapaswa kutazama ni wapi tunaweza kuanzia kukabiliana na suala hili. Ukiwasikiliza Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA) wanaonyesha suluhu yao ya matatizo haya kuwa si kumbebesha mzigo dereva lakini kuna haja ya kuwapatia mikataba madereva hawa yenye tija katika hali zao za kila siku. 

Pia hatupaswi kuachia tu njia za usafirishaji mfano wa barabarani kwa watu binafsi tu, lazima kuwepo na ushirika wa madereva, wawe na umiliki wa magari yao wenyewe, wasiwe na wasiwasi na mishahara yao, na posho zao kama ilivyo sasa. Madereva hao wana shaka na kesho yao, wanaishi kwa posho tu, wanakimbiakimbia barabarani kufukuzana na posho.  

Badala ya dereva kutafutwa na posho sasa dereva anaitafuta posho. Ndipo tulipofikia. 

Rai yangu

Kwa wadau wa usalama wa barabarani na watafiti wa masuala ya ajali, ni muhimu kutumia lenzi mpya ya kutazama hali halisi ya maisha ya watu na kuyapatia tafsiri ya tatizo la ajali za barabarani. Hapo tunaweza kuanzia kuhusu kukabiliana na tatizo hili. 

Lakini kama tutaishia kudhani kwamba elimu na kukagua magari pekee inatosha, sisemi elimu si ya muhimu au ukaguzi wa magari si muhimu, la hasha!

Ni muhimu lakini muhimu zaidi ni kwenda kutafuta kiini cha tatizo hili, tuanzie katika mizizi kwenye masilahi ya dereva na bosi wa chombo husika.

Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).

0659-639808/0683-961891

[email protected] 

By Jamhuri