Bashir  Yakub

Kwanza; ukinunua ardhi (nyumba, kiwanja, shamba) hakikisha unafanya ‘transfer’ (kuhamisha umiliki kutoka aliyekuuzia kwenda jina lako, mnunuzi) mara moja kadiri uwezavyo.

Wengi mkinunua kwa sababu hakuna anayekulazimisha kufanya ‘transfer’ kwa haraka, basi mkishakabidhiwa hati na mikataba ya mauziano mnakaa nazo hata miaka miwili au mitatu mkisema: “Nikipata hela ndipo nitakapofanya ‘transfer’.” Usifanye hivyo!

Mjue kuwa kama hujafanya ‘transfer’ uwezekano wa aliyekuuzia kukuzunguka na kukuchezea ni mkubwa sana.

Mfano mmoja ni kuwa, aliyekuuzia anaweza kutoa taarifa ya kupotelewa hati, hivyo kupatiwa taarifa ya kupotea (lost report).

Kisha, akafanya tangazo katika gazeti la kawaida na lile la Serikali (GOVERNMENT GAZETTE@GN).

Kisha, akafanya maombi ya kupatiwa hati mpya kupitia Form No. 3 chini ya Kifungu cha 38 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334.

Kisha, atapatiwa hati nyingine mpya. Kwa hiyo kutakuwa na hati mbili katika ardhi moja, ile aliyokupa wewe mnunuzi na hii mpya ya kwake.  

Huu tayari ni mgogoro mkubwa kwako mnunuzi usiye na hatia (bonafide purchaser).

Akishakuwa na hati, hayo mengine anaweza kuyakataa kirahisi, na pengine watu wa namna hii hata zile saini anazokuwa amekuwekea kwenye nyaraka nyingine zinakuwa si zake. 

Lakini mbaya zaidi ni kuwa, usipofanya ‘transfer’ na wakati umeshanunua, shughuli zote zinazohusu ardhi hiyo, mfano kulipia kodi za ardhi, vibali vya ujenzi, tathmini, tozo na kila kitu kinaendelea kusoma jina la aliyekuuzia na kinafanyika kwa jina la aliyekuuzia.

Maana yake ni kwamba, ushahidi wote wa risiti na nyaraka nyinginezo unaendelea kumtambua aliyekuuzia kuwa mmiliki halali ambapo anaweza kutumia ushahidi huo dhidi yako. 

Ataonyesha risiti zinamsoma yeye na atasema nilikuwa nalipia, atachukua hata kibali cha ujenzi bila wewe kujua na atakionyesha kinamsoma yeye nk.  

Ndugu yangu, wewe hapo kutoboa katika mazingira hayo unahitaji tu kudra za Mwenyezi Mungu kama utabahatika kuzipata.

Lakini kama umefanya ‘transfer’, mchezo huu ni mgumu sana na pengine usiowezekana, na hata ukiwezekana kwa nguvu ya rushwa au mamlaka bado unaponyeka (curable) kwa sababu mfumo huonyesha umiliki ulivyokuwa ukihama hadi mmiliki wa mwisho.

Ninachotaka kuwashauri mkafanye ‘transfer’ haraka mnaponunua. Najua mnaogopa gharama hasa ‘Capital Gain’ ambayo ni asili. Lakini hii mbona inazungumzika na huwa inapungua? 

Hata hivyo mna uhuru wa kuchagua kati ya shari kamili ya kudhulumiwa ardhi yote au nusu shari ya hiyo asilimia 10. 

Pili; mkinunua hakikisha mikataba yenu inashuhudiwa na mawakili. Nimeona ule wa Makonda na Gharib ulishuhudiwa na Wakili aitwaye Ibrahim Shineni. 

Huyu kwa sasa ni nguzo muhimu mno. Yaani mno katika huu mgogoro.

Wakili kwa cheo chake ni ofisa wa viapo (Commissioner for Oaths), ni Mthibitishaji wa Umma (Notary Public)  pia ni Ofisa wa Mahakama.

Akiwa kwenye mkataba wako wa manunuzi ya ardhi ni mtu muhimu mno na shahidi wako muhimu anayeaminiwa sana na Mahakama. 

Basi haya mawili yakufunzeni.

By Jamhuri