*Profesa Silayo apania kurejesha uoto wa asili Kanda ya Ziwa, huku akiifanya Dodoma kuwa ya kijani

MAGU

Na Joe Beda

Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) umedhamiria kurejesha uoto katika maeneo ya nyanda kame (dry land areas) nchini, ikiwa ni kutekeleza maagizo ya serikali.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Utalii, Mary Masanja, aliyekuwa mgeni rasmi wa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa kwa mwaka huu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba mjini Magu wiki iliyopita.

Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yamefanyika sambamba na Siku ya Misitu Duniani, na mgeni rasmi, Naibu Waziri, Mary, katika hotuba yake amewaelekeza TFS na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) kuanzisha bustani ya kitalu cha miche ya miti itakayohudumia Wilaya ya Magu na maeneo mengine ya nyanda kame yanayozunguka Ziwa Victoria.

“Hii itasaidia miche kupatikana kwa wingi, kwa kuwa sasa wananchi wana hamasa ya kupanda miti,” anasema Mary na kuongeza kuwa ni kazi ya TFS na TaFF kubaini maeneo sahihi ya kupanda miti pamoja na kutoa elimu ya ugani kwa wananchi ili miti iliyopandwa itunzwe na kudumu.

Awali, Naibu Waziri alizindua kampeni ya upandaji miti maeneo ya nyanda kame kwa yeye na viongozi wengine wa serikali kupanda miti kwenye eneo la Shule ya Msingi Sagani iliyopo nje kidogo ya mji wa Magu.

Kwa kutambua ukweli kwamba Magu na wilaya kadhaa za Kanda ya Ziwa zinanyemelewa na ukame, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, anasema:

“Pamoja na kupaza sauti kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu, TFS tutaendelea kuboresha uhifadhi huo ukiendana na matumizi endelevu ya misitu. 

“Tunaposema ‘matumizi endelevu’ tunamaanisha kuwapo kwa upatikanaji wa bidhaa za misitu bila kuiathiri misitu yenyewe.” 

Anasema misitu ya kupanda itawasaidia wananchi kupata bidhaa za misitu na kupunguza utegemezi wa misitu ya asili iliyopo katika hatari ya kutoweka.

Maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti na Siku ya Misitu Duniani mwaka 2022 yamepambwa kwa kaulimbiu ya ‘Mti Wangu, Taifa Langu, Mazingira Yangu, Kazi Iendelee’, yakilenga kurejea uoto wa asili uliotoweka katika maeneo kadhaa ya Ziwa Victoria.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ‘upandaji miti, utunzaji wake na matumizi endelevu ya mazao ya misitu’,” anasema Profesa Silayo.

Maeneo ya nyanda kame yanajumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu pamoja na mengine ambayo yamepoteza uoto wa asili, historia ikionyesha kuwa hali hiyo imetokea baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. 

Takwimu zinaonyesha kuwapo kwa uoto mdogo wa misitu katika mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa tofauti na maeneo mengine nchini.

“Miti na misitu iliyokuwapo awali ilikatwa na wananchi kufukuza wadudu kama mbung’o waliokuwa wakidhuru mifugo yao. Bahati mbaya hawakupanda miti mingine.

“Sasa TFS katika siku hii tunapaza sauti na kuwapa wananchi elimu juu ya umuhimi wa kurejesha uoto uliotoweka na kuendeleza uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu,” anasema Profesa.

Miongoni mwa mbinu zinazopangwa kutumiwa na TFS ni kushirikisha taasisi kama shule na vyuo kupanda miti na kuitunza.

Kama maji ni uhai, basi miti ndiyo asili ya uhai wenyewe; na Profesa Silayo akizungumza kuhusu Wiki ya Maji na uhusiano uliopo na misitu, anaeleza namna misitu inayohifadhiwa na TFS inavyochangia upatikanaji wa maji nchini.

“Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya hifadhi ya maji na misitu, kwa sababu maji yanapatikana katika maeneo yanayoitwa ‘water catchment’ (madakio ya maji) na misitu mingi yamekuwa ni madakio mazuri ya maji,” anasema Profesa Silayo.

Anautaji mtandao wa Misitu ya Tao la Mashariki kama eneo linalowapa maji robo ya wananchi wa Tanzania, hivyo kuonyesha umuhimu wa kuihifadhi misitu hiyo ili kuendelea kupatikana kwa maji.

Profesa Silayo ndiye aliyesimamia uanzishaji wa shamba la miti la pili kwa ukubwa nchini liitwalo ‘Shamba la Silayo’ mkoani Geita.

Kwa sasa mtaalamu huyu wa uhifadhi amepania bila hofu yoyote kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

By Jamhuri