Baada ya matokeo ya mitihani ya darasa la VII ya mwaka 2011 kutangazwa, kumetokea tashtiti kubwa katika nchi hii. Kule kutangazwa kwamba wanafunzi 5,200 hawajui kusoma wala kuandika, lakini wamo miongoni mwa watoto 567,567 waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu, kumewashangaza wengi. Naona kama ni jambo fulani la kisanii!

Mwaka 2011 tumesherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Taifa letu na kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana. Katika elimu tumesikia maelfu ya watoto wetu hawajui kusoma wala hawawezi kuandika, na si hivyo tu, bali wameteuliwa kujiunga na masomo ya sekondari! Ni maajabu ya mwaka haya!

 

Idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2011 ni 983,545, wakiwamo wasichana 287,377 na wavulana 289,190. Miongoni mwa hawa ndimo tulimosikia watoto 5,200 ni ‘vihiyo’, yaani hawajui kusoma wala kuandika!

 

Zimetolewa sababu kadhaa kwa hali hii. Wengine wanasema usimamizi wakati wa mitihani umekuwa mbovu, na hicho ni chanzo kimojawapo cha wasio na sifa kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari. Hayo yalitolewa na Fredy Azzah katika gazeti moja la kila siku la Jumanne Agosti 28, 2012.

 

Lakini NGO moja jijini Dar es Salaam licha ya kusanifu ubora wa elimu ya nchi hii kwa lile tangazo la “Shule ya janja janja” inayofaulisha watoto wote kwa mbinu za kuhonga wasimamizi wa mitihani, wametoa maoni mazuri tu katika gazeti hilo hilo. Wamesema, “Tuyapimeje mafanikio katika sekta ya elimu?” Wamesema, “Kwa muda sasa Tanzania imeendelea kutajwa kuwa nchi yenye viwango duni vya elimu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Hii inatokana na uwezo wa wahitaji katika soko la ajira, ubora wa maarifa yanayotolewa, viwango vya ufaulu na idadi ya wahitimu katika vyuo vya elimu ya juu. Haya ni matokeo ya mtafiti Makumba Mwemezi. Ni maoni yakinifu yatokanayo na utafiti wa kisayansi.

 

Kuongezeka kwa watoto wanaosoma katika shule za msingi, sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu, au kuongezeka kwa shule na vyuo hapa nchini hakumaanishi ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wetu wa Tanzania.

 

Ndipo lilipozuka swali kwamba kama shule zetu zinatoa elimu bora inakuwaje idadi ya wazazi wenye uwezo kifedha, wanaacha kupeleka watoto wao katika hizi shule za wananchi katika kata zao au mikoa yao, lakini wanakubali kugharamia watoto wakasome shule za watu binafsi na vyuo vya nje ya nchi imeongezeka?

 

Najiuliza huko kinafuatwa nini? Jibu la haraka haraka kutoka kwangu ni kuwa wanafuata elimu bora! Ala! Kumbe hapa kwetu haipo hiyo elimu bora? Sasa huu mfumo wa elimu ya ubaguzi umeanzaje katika nchi hii ya kijamaa?

 

Wale waliosoma kitabu cha riwaya cha George Orwell “The Animal Farm” (Bridge series) watakumbuka kuwa “Animal Farm” lilikuwa shamba la mifugo ya mtu lenye wanyama wote na waliokubaliana kuishi kijamaa, kufanya kazi pamoja kwa faida ya wote na kugawana matunda ya kazi zao sawa sawa kwa wanyama wote.

 

Ndipo wakajitungia kanuni za kuishi katika umoja wao huo katika shamba lile huku wote wakikubaliana kumpinga mwanadamu, bwana mwenye shamba lile kuwa ni mnyonyaji na wala si mwenzao!

 

Labda kwa faida ya wasomi vijana wasiojua siasa yetu ile ya Ujamaa na maisha katika Vijiji vya Ujamaa niwamegee kidogo kuwa sheria za mle shambani zilikuwa saba, nazo zilisomeka hivi;

 

The seven commandments (Uk 16 wa Animal Farm)

1.      Whatever goes upon two legs is an enemy.

2.      Whatever goes upon four legs or has wings is a friend

3.      No animal shall wear clothes

4.      No animal shall sleep in a bed

5.      No animal shall drink alcohol

6.      No animal shall kill another animal

7.      All animals are equal

Kwa tafsiri ya amri hizo ni kwamba:

1. Yeyote atembeaye kwa miguu miwili ni adui

2. Yeyote atembeaye kwa miguu minne au mwenye mbawa ni rafiki

3. Ni marufuku mnyama kuvaa nguo

4. Ni marufuku mnyama kulala katika kitanda

5. Ni marufuku mnyama kutumia kileo

6. Ni marufuku mnyama kuua mnyama mweziwe

7. Wanyama wote ni sawa

 

Wanyama wale walikubaliana waitane “ndugu” wala pasiwepo mnyama wa kuitwa “bwana” kwani wote walikuwa ni sawa kabisa! Basi, ikajitokeza aina moja ya wanyama ikawa “janja” na kuwazidi akili wanyama wengine wote.

 

Wakajitengenezea utaratibu wa kufaidi zaidi matunda ya zile kazi za mle shambani, mathalani kupata chakula zaidi, kusimamia kazi na si wao kuchapa kazi. Hatimaye aina ile wanyama ikazifuata zile sheria zote saba za katika shamba lile na kutoa amri moja tu iliyosomeka hivi “All animals are equal but some are more equal than others.”

 

Hapakuwa na ubishi wala tafsiri nyingine yoyote isipokuwa aina ile ya wanyama ikawa watawala na wanyama wengine wote wakabaki vibarua watawaliwa! (UK 92 wa Animal Farm). Kwa nini nilete mfano huu? Swali lile la watafiti wa NGO moja hapa nchini kuwa kama elimu yetu inafaa kwa watoto wote katika nchi hii ya Ujamaa, inakuwaje matajiri (vigogo) wanapeleka watoto wao shule za binafsi au nje ya nchi? Hizi shule zetu tulizojenga wananchi (community schools) katika mikoa, tarafa na kata zetu ni kwa ajili ya watoto wa akina nani?

 

Kumbe zipo shule na shule; ile Siasa ya Ujamaa ilishazikwa pamoja na Azimio la Arusha na hivyo kuna watu na watu! (Some people are more equal than others) – watoto wao kamwe hawawezi kusoma katika shule za kata.

 

 

 

 

By Jamhuri