Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas, amewatahadharisha wanafunzi kuacha tabia ya kupokea zawadi kutoka kwa watu wasiowajua ili kuepuka kufanyiwa vitendo vya kikatili.
Kanali Thomas ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Muhuwesi iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma.
“Zawadi nyingine zinaweza kuwa na nia mbaya ya kuwaharibia masomo na maisha yenu kwa sababu mnaweza kufanyiwa vitendo vya kikatili’’amesisitiza.
Amewataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kukataa vishawishi vinavyoweza kuwasababishia kufanyiwa vitendo vibaya na kwamba yeyote ambaye atafanyiwa vitendo hivyo atoe taarifa haraka kwa wazazi na walimu ili hatua zichukuliwe kwa muhusika.
Kanali Thomas amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili baadae waweze kulitumikia Taifa kwa weledi na kuwa wanajamii bora wanafuata maadili mema ya kitanzania.
Katika hatua nyingine Kanali Laban Thomas ametoa msaada wa mifuko ya saruji 28 inayogharimu Zaidi ya shilingi 420,000 kwa ajili ya kuweka sakafu katika vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Muhuwesi.
RC Thomas amemuagiza Meneja Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Tunduru kuhakikisha shule hiyo inaunganishiwa huduma ya maji ya bomba ili kuwapunguzia wanafunzi kubeba ndoo za maji toka nyumbani kwa ajili ya shughuli za usafi na mazingira ya shule.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameshakagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa wa Ruvuma ambapo katika wilaya ya Tunduru aliongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro.