Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Anne Makinda amewataka waandishi wa habari kutumia matokeo ya sensa kuandika habari zitakazosaidia katika uboreshaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Amebainisha hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mafunzo ya siku mbili kwa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) kuhusu matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na jinsi ya kuyatumia matokeo ya Sensa katika kuandika habari.
Makinda ambaye pia ni Spika Mstaafu, amesema waandishi wa habari ni watu ambao wanawategemea katika kuwafikishia wananchi matokeo ya Sensa pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa wake katika kukuza Maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
“Waandishi wa habari mna nafasi kubwa katika suala hili na sisi tunawategemea. Tunategemea nchi yetu ifike mahali inazungumza habari za takwimu, sio tunazungumza maneno ya majungu majungu tu vitu vitu visivyoeleweka, hapana, tuzungumze maendeleo.
“Hivyo kwa sasa ni wakati wa kuyafikisha Matokeo ya Sensa kwa wananchi ili waweze kuyatumia kwa ajili ya mipango yao ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii,” amesema Makinda.
Ameongeza kuwa baada ya Rais kutangaza matokeo ya mwanzo mwaka 2022, kulitokewa mwongozo ambao lengo lake kuu ni kutumia matokeo ya sensa ya mwaka 2022 ili kuongeza uelewa, kufanya uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa serikali.
Ameongeza kuwa taarifa za Sensa ni muhimu kwa wananchi pia na wadau wote ili waweze kupanga mipango yao jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na mazingira.
Sambamba na hayo amewataka wanasiasa kutofurahia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, badala yake watambue kuwa inaweza kuwa kiboko kwao kwani wananchi watakuwa na uelewa wa kutosha.
“Nawaambia wanasiasa wenzagu, sensa hii imefanikiwa. Lakini, kwenu ni kiboko, shangilieni lakini watu watakuwa wanauliza maswali kutokana na takwimu na maelezo yaliyomo kwenye matokeo ya sensa. Sisi tunafundisha mpaka chini kwa wananchi,” amesema Makinda.
Hata hivyo amesema kutokana na wananchi kupata uelewa kuhusu matumizi ya takwimu ikitokea kiongozi wa siasa anataka kusema vitu vyake visivyo na uhalisia, wananchi watamhoji kwani uelewa kuhusu umuhimu na matumizi ya takwimu za sensa wanaijua.