Na. WAF – Mwanza

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezitaka Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini kuanza kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo leo Machi 14, 2024 wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mwenyekiti Mhe. Stanslaus Nyongo iliyotembelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekotoure) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ambapo kwa ujumla Kamati imeridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali hizo.

“Katika Hospitali hii ya Bugando hakuna mtu anaebeba karatasi, kuanzia mteja anaingia kumuona daktari hadi anatoka, tunataka Hospitali nyingine ziige ziweze kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi, tunataka mteja akija asikae zaidi ya masaa Matatu.” Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutambua na kuthamini michango ya Taasisi za Dini katika utoaji wa huduma za Afya kwa watu wa Kanda ya ziwa ikiwemo Hospitai ya Bugando.

Amesema, mbali na jitihada za Serikali katika kuongeza watumishi wa Sekta ya Afya, Halmashauri, Hospitali ziajiri watumishi wa mikataba ili kupunguza changamoto ya watumishi na kuongea kasi ya upatikanaji wa huduma za Afya nchini.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya afya na ninyi wenyewe ni mashahidi katika hili, tunaendelea kupambana na changamoto za ubora wa huduma ambalo ni kwetu sisi watumishi pamoja na ugharamiaji wa huduma za Afya.” amesema Waziri Ummy.