Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wahandisi washauri wababaishaji ambao wameshindwa kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara na kupelekea kuharibika kabla ya wakati.
Ameeleza, wahandisi hao wamekuwa wakiisababishia hasara kubwa Serikali kwa kukosa kusimamia kikamilifu miradi hiyo.
Agizo hilo limetolewa machi 22, 2024 wilayani Mafia katika ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo .
Aidha ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kutowapa kazi makampuni ambayo yameisababishia hasara Serikali katika miradi ya barabara.
“Niagize TANROADS kuwaweka kwenye black list makampuni ya wasimamizi wa mradi waliovurunda kwenye usimamizi wa miradi ya barabara hapa nchini na ikitokea barabara imeharibika kabla ya wakati ,Mkandarasi na Mhandisi Mshauri warudie kwa gharama zao kwa mujibu mkataba”, amesisitiza Bashungwa.
Vilevile Bashungwa amekagua ujenzi wa barabara ya Kilindoni – Utende yenye urefu wa (km 14.6) iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara ya Kilindoni – Rasmkumbi yenye (km 52.28) ambapo tayari (km 2.2) zimeshajengwa kwa kiwango cha lami .
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi hiyo ili kuifungua Wilaya ya Mafia kwa miundombinu ya barabara bora na ya uhakikia wakati wote.
“Lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kuifungua Mafia kiuchumi hivyo anatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara wilayani hapa, ni lazima tusimamie miradi ambayo inatumia fedha nyingi za Serikali” anasema Bashungwa
Bashungwa ameeleza, mkakati wa Serikali uliopo ni kuanza taratibu za kumpata Mkandarasi ili kuweza kujenga kipande kilichobaki cha barabara ya Kilindoni – Rasmkumbi takribani kilometa 50.
“Kwa sababu ya jiografia ya Mafia tukiijenga vipande vipande hatutapata tija na kutakuwa na gharama zaidi kutokana na namna ya kupata vifaa vya ujenzi hivyo ni lazima tulete Mkandarasi mmoja ili akiianza barabara hii abaki Mafia hadi barabara hiyo ikamilike”, amefafanua Bashungwa.
Nae Meneja wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Pwani , Mhandisi Baraka Mwambage anasema ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 52 kutoka Kilindoni hadi Rasmkumbi inakwenda kufungua uchumi wa kisiwa cha mafia ,kukuza sekta ya utalii na kurahisisha usafiri maeneo ya wakulima yaliyopo Rasmkumbi