Askofu mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Daniel Mono amewataka wananchi wa Wilaya ya Mwanga kuyashika na kuyaenzi mambo makuu manne aliyoyaacha Cleopa Msuya.
Askofu Mono amesema Wilaya ya Mwanga ilipata kiongozi na mbunge bora aliyewapenda wananchi wake na kutumia maisha yake katika maendeleo ya Mwanga na taifa kwa ujumla.
Askofu Mono alisema hayo jana akitoa mahubiri baada ya kuongoza sala takatifu ya kumwombea aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Msuya.
“Msuya katika maisha yake alisema kile alichokiamini na alitenda kile alichokiamini, alikuwa muumini bora aliyesema kile kinachofanana na uso wake. Imani aliyoiishi akiwa mtumishi wa umma ndiyo aliyoiishi akiwa kanisani,” alisema Askofu Mono.
Alisema taifa linastahili kumshukuru Mungu kwa sababu Msuya alikuwa mwalimu kwa wote na kuwataka Watanzania kuyaishi na kuyaendeleza mazuri aliyoyaacha kama urithi wa taifa.
Aliongeza kuwa Mungu alimtumia Msuya kuleta mwanga ndani ya Mwanga na taifa kwa ujumla na kwamba amewaachia wananchi wa Mwanga umoja na mshikamano.
Alisema jambo lingine ni kuishi katika umoja, mshikamano na upendo kama alivyowajenga wananchi wake kwani kwa kufanya hivyo ataifurahia safari yake ya kwenda kwa Mungu wake.
“Ameiacha Mwanga salama yenye umoja na mshikamano bila kujali tofauti ya kidini. Viongozi waige maisha ya Msuya waweke maslahi ya taifa mbele, tutosheke na mishahara yetu na pia wana Mwanga msikubali kugawanyika na badala yake tuwe kitu kimoja,” alisema Askofu Mono.
Aliongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kuyaiga maisha yake kwa kusema kweli na kukataa uongo pamoja na hongo ili kuchagua viongozi kwa sababu kwa kufanya hayo ni kuuza utu wao.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza akitoa salamu za shukrani, aliishukuru serikali kwa kumpa heshima kubwa Cleopa Msuya hali iliyoipa heshima kubwa Wilaya ya Mwanga na Kilimanjaro kwa ujumla.
Alieleza kuwa kutokana na heshima hiyo ni wazi kuwa inakosekana tofauti kati ya Waziri Mkuu aliyestaafu na aliyepo kazini.
Alimtaja Msuya kuwa katika utumishi wake ameacha alama kubwa kwa kujali maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.
