Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Leo naanza makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Dunia kwa kunipa uhai na fursa nyingine ya kuandika makala hii. Wiki iliyopita niliandika makala nikipinga juu ya kupotea kwa Mdude Nyagali na kuvamiwa kwa Padre Dk. Charles Kitima. Nikiri makala hii imeniletea ujumbe mwingi wa pongezi na kunitia moyo niendelee na ujasiri wa kuandika ukweli.
Nishukuru pia kuwa Mei 5, 2025 nilipata Tuzo ya Wizara kwa uandishi wa habari za siasa uliotukuka. Hii nayo imeniletea pongezi nyingi na za aina yake. Wapo watu wamenikumbusha makala zangu za hadi mwaka 2000 wakati naandika safu ya SIASA WIKI HII katika Gazeti la Mwananchi. Niliibadili safu hii na kuiita SITANII, baada ya kubaini watu mbalimbali walianzisha safu na kuziita SIASA WIKI HII, bila kujali kuwa mwanzilishi wa safu yupo.
Sitanii, kwa hakika wiki iliyopita ilikuwa ni wiki ya pongezi. Pamoja na mimi Deodatus Balile, wengine waliopata tuzo hii ya umahiri katika kuandika habari za siasa zenye kuunganisha taifa ni Abasalom Kibanda, Mbaraka Islam na dada yetu Hawra Shamte. Namshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia tupewe tuzo hizo, nawashukuru waandaji Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCA).

Kwa kweli tuzo hizi zilifana na kwa mara ya kwanza zimekutanisha waandishi wa habari kutoka kila kona ya nchi hii wakongwe kwa vijana. Nikiri jukumu alilotupatia Mhe. Rais Samia kuwa sisi tuwe walezi wa vijana wakue kitaaluma, hakika tutalifanya kwa unyenyekevu mkubwa. Ni kweli vyombo vya habari tunalo jukumu la kusaidia wananchi kujiletea maendeleo badala ya kila siku kuandika upande mmoja tu wa shilingi, mabaya ya serikali.
Sitanii, baada ya usuli huo, sasa najielekeza katika kukishauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Chama hiki nimekishuhudia tangu kinasajiliwa na awamu zake za ukuaji. Nitangulie kusema litakalotokea. Kuna baadhi ya wafuasi wa CHADEMA wanapenda kusikia upande mmoja tu, hapa ninachokwenda kukiandika nimejiandaa watafuta pongeze karibu zote walizonipa wiki iliyopita, na kuporomosha matusi.
Nasema nimekishuhudia CHADEMA tangu kinaanzishwa Mei 28, 1992, na kupata usajili wa kudumu miaka 32 ilipopata yaani, Januari 21, 1993. Mwenyekiti wake alikuwa Mzee Edwin Mtei. Hakikusimamisha mgombea urais mwaka 1995 au mwaka 2000. Mwaka 1998 Mzee Bob Makani alichaguliwa kukiongoza chama hicho. Mwaka 2004 Freeman Mbowe alichaguliwa na 2025, Tundu Lissu akachaguliwa.
Sitanii, naikumbuka CHADEMA ambayo ilikuwa tunakwenda kuripoti habari zake Kanda ya Ziwa tukiwa na akina Mzee Philemon Ndesamburo, Jomba Coy, Jacob Nkomola, Grace Kiwelu, Freeman Mbowe, Shaibu Akwilombe na wengine ambao tulifika Tarime tukakutana na akina Mama Vivian na Rasta Chacha Wangwe wakiwa Diwani wa NCCR-Mageuzi, ila usiku huo mwaka 2005 wakahamia CHADEMA.
Chama hiki hakikuwa tishio hata chembe. Mwaka 1995 NCCR-Mageuzi ndiyo walikuwa tishio chini ya Agustino Lyatonga Mrema aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, maarufu kama Mzee wa Kiraracha. Mwaka 2000 napo kilikuwa bado (nitatoa takwimu). Mwaka 2005 kilianza kushitua mbavu baada ya Freeman Mbowe kugombea urais wa Tanzania. Idadi ya wabunge kwa vyama vyote vya upinzani ilikuwa kama ifuatavyo:-
Mwaka 1995 CUF ilipata wabunge wengi Zanzibar (25), NCCR (19) – nitataja majina haya ya wabunge hawa wa kwanza wa NCCR-Mageuzi, ambayo naona watu wanayachanganya, ila leo katika makala hii nitaweka kumbukumbu sawa kuthibitisha ukongwe na umahiri katika habari za siasa kuepusha nchi yetu isipoteze historia hii muhimu.
Sitanii, kwa nia ya kusaidia kumbukumbu, naomba nikiuke kidogo misingi ya uandishi nitumie namba kabla ya kila jina kukusaidia kuhesabu vyema. Wabunge hawa walikuwa ni 1. Masumbuko Lamwai (Ubungo), 2. Augustine Lyatonga Mrema (Temeke), 3. Mabere Marando (Rorya), 4. James Mbatia (Vunjo), 5. Mutamwega Mugaywa (Mwibara), 6. Stephen Wassira (Bunda) na 7. Makongoro Nyerere (Arusha Mjini).
Wengine ni 8. Polisya Sikumbula Mwaiseje (Mbeya Mjini), 9. Mfwalamagoha Kibasa (Iringa Mjini), 10. Makidara Mosi (Siha), 11. Dk. Jacob Msina (Urambo Mashariki), 12. Jerald Ngotorainyo (Moshi Vijijini), 13. Ndimara Tegambwage (Muleba Kaskazini), 14. Mwinyihamisi Mushi (Hai), 15. Joseph Mtui (Moshi Mjini) na 16. Paul Ndobho (Musoma Vijijini).
Idadi ya wabunge hawa wa kihistoria wa upinzani 16 wa majimbo, ilikamilishwa na wabunge watatu wa viti maalum ambao ni 17. Edith Lucina, 18. Exaveria Nchimbi na 19. Chiku Abwao. Wakati huo Chadema ilipata wabunge wanne (4) na UDP watatu (3). Jumla Bunge la Mwaka 1995 ilikuwa na wabunge wa upinzani 51.

Mwaka 2000 idadi ya wabunge wa upinzani ilishuka. CUF walipata wabunge 21, Chadema (5) hivyo kufanya idadi ya wabunge wa upinzani kuwa 26. Unafahamu nini kiliwashusha NCCR-Mageuzi? Ni mgogoro kati ya Mrema na Marando ambao ulikiacha chama hoi. Mwaka 2005 idadi ya wabunge wa upinzani ilipanda tena na kufikia 41. Zamu hii CUF walipata wabunge 30 na Chadema 11.
Sitanii, wapinzani walianza kuaminika kwa wananchi. Mwaka 2010 CUF waliongeza idadi ya wabunge na kufikia 48, Chadema wakapanda hadi 36, NCCR-Mageuzi ikapata wabunge watano (5). Jumla ndani ya Bunge kukawamo wabunge 89 wa upinzania. Mwaka 2015 ilikuwa kilele. Idadi ya wabunge wa upinzani iliongezeka na kufikia 114. CHADEMA walipata wabuunge 70, CUF (42), NCCR Mageuzi (1), ACT Wazalendo (1).
Kilichotokea baada ya hapo yaani mwaka 2020 ni historia nyingine. Kutoka wabunge 114 bungeni, idadi ya wapinzani ilishuka hadi wabunge wanane (8) na wakiwekwa wale wa Viti Maalum 19 wa Chadema wasiotambulika ikawa 27. Katika uchaguzi huo ambao wapinzani waliambiwa hawajui kusoma wala kuandika CUF walipata wabunge watatu (3), Chadema (1) na ACT Wazalendo (4).
Sitanii, nafahamu wengi mnajua migogoro ilivyoua vyama vya upinzani, ukiacha kimbunga cha utawala usiokubalika cha mwaka 2020 kilichonuia kuua upinzani kwa makusudi. Naamini kama ni mafundisho tumekuwa nayo ya kutosha kutoka mgogoro wa Mrema na Marando, hadi mgogoro wa Prof. Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Shariff Hamad.
Hata kama kuna madai ya kuwapo mkono wa chama tawala katika kusambaratika kwa vyama hivi, najiuliza vyenyewe inakuwaje visione viashiria na kuziba matundu? Nirejee kwa CHADEMA. Mwaka 2000 chama cha Chadema hakikuwa na mgombea wa urais. Mwaka 2005 mgombea wa Chadema Freeman Mbowe alishika namba tatu kati ya wagombea kumi akapata asilimia 5.88 za kura.
Mwaka 2010 Chadema ilipata asilimia 27.1% na mgombea urais wa chama Dk. Wilbrod Peter Slaa akapata kura 4,627,923 sawa na 31.75%. Mwaka 2015 mgombea wa Chadema alikuwa Edward Ngoyai Lowassa aliyehama CCM baada ya kukatwa jina. Dk. John Magufuli wa CCM alipata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46 na Lowassa alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97.
Sitanii, ukiacha ajali ya kisiasa ya mwaka 2020, unaona bayana kuwa kwa mwenendo huu CHADEMA kilikuwa chama kinachokua kisiasa. Ni wazi kuwa matukio yaliyopita, hayakuwa ya kiungwana kwa kiwango cha kukatisha tamaa yeyote awaye kwa mwaka 2020. Hata hivyo, mchezo wa siasa ni sawa na mambo ya nyakati.
Niseme jambo hapa, kuwa siasa si mchezo wa kiharakati, bali ni mchezo wa mchakato. Ukifanya harakati katika siasa unapoteza kila kitu. Msingi mkuu wa kufanya siasa ni kujega urafiki na kuaminika kwa pande zote mbili. Hata kama ni chama tawala, kinapaswa kuaminika kwa wapinzani na chama cha upinzani kinapaswa kuaminika kwa wafuasi wa chama tawala ikiwezekana na viongozi wao na mifumo ya kuongoza nchi.
Siasa haziendi na upepo wa matukio, hizo ni harakati. Utaona wakati Tanganyika inapigania Uhuru, pamoja na kwamba Mwalimu Julius Nyerere alikuwa anawapinga kwa kiwango cha juu wakoloni, bado alikuwa anafunga safari anakwenda Umoja wa Mataifa, anakwenda Lancaster House Uingereza kufanya majadiliano nao. Ukiishakuwa na mkakati, kwenye siasa ukiona mkakati unaelekea kufanya kazi, basi hapo hapo unakimbilia maridhiano. Hii inaleta kuaminika.
Kwa bahati mbaya, narudia, kwa bahati mbaya, viongozi wa CHADEMA, wamechukulia siasa kama harakati za matukio. Wamedhani siasa ni sawa na kufanya harakati kuwa watu wamefukiwa kwenye mgodi wa Bulhyanhulu, wafadhili wakatoa matamko na kusambaza ripoti duniani kote, kama NGO ikaweka tiki kuwa imefanikisha harakati.

Siasa ni kujenga mizizi. Ifike mahala, Kamanda wa Polisi amwelewe kiongozi wa upinzani, kwamba kwa kweli katika hili anayo hoja na inazunguzika. Kuongoza chama cha siasa si sawa na urais wa serikali za wanafunzi, ambapo yakipikwa maharage yenye wadudu, rais wa wanafunzi anawahamasisha wenzake siku hiyo hiyo wanaandamana. Wanasahau na jukumu la msingi lililowapeleka chuo, wanasusa si chakula tu, bali na masomo na kuvunja vioo vya mabweni!
Kwa siku za karibuni nimewafatilia Chadema. Nimefatilia kaulimbiu yao ya No Reforms, No Elections (Bila mabadiliko hakuna uchaguzi). Ni kweli kwamba uchaguzi wa 2019, 2020, 2024 kila awaye aliutilia shaka. Tukumbushane kuwa mwaka 2019 Uchaguzi wa TAMISEMI ulisimamiwa na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, 1979.
Mwaka 2020 Uchaguzi Mkuu ulisimamiwa chini ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, 1985. Mwaka 2024 Uchaguzi wa TAMISEMI Umesimamiwa na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, 1979. (HAIJABADILISHWA). Ukweli usiosemwa kwa wapiga kura ni kuwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 imefutwa haitatumika mwaka 2025. Hili lilikuwa dai la msingi la CHADEMA, ila ukweli huu hausemwi na wanaofanya harakati.
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 utasimamiwa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani (NI SHERIA MPYA). Wanaopinga hawaitaji popote hii kuwa kuna mabadiliko yaliyofanywa. Sheria hii inaziba mianya iliyokuwapo ikiwamo mgombea kupita bila kupingwa, imefutwa. Yapo mabadiliko mengi tu ndani ya sheria hii.
Mwaka huu kuna Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) (HII NI SHERIA MPYA), hii ni tofauti na Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoanzishwa chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977). Wajumbe wa INEC wanapaswa kuomba hii kazi na si kuteuliwa kama zamani. Nilitaraji hapa hoja iwe kuwabana wakubwa kutangaza mchakato wa kuunda Tume Huru kwa mujibu wa sheria, ila si kudanganya umma kuwa hayajafanyika mabadiliko.
Kuna madai kuwa Tume Huru ya Taifa iwe na wafanyakazi (waajiriwa wake) kwani watumishi wa umma hawaaminiki. Hii ni hoja dhaifu, kwani inarudi palepale. Hazina ambayo ni Serikali ndiyo itakayowalipa mishahara hawa watumishi wa Tume. Pia ikumbukwe kwa miaka 5 watafanya kazi miezi mitatu hadi sita kwani si wakati wote ni wa uchaguzi. Kama tatizo ni uadilifu wa watumish wa umma, tushughulikie hilo.
Tatizo hapa ni moja. Pande zote ziseme ukweli. Kudai hakuna mabadiliko yaliyofanywa, wakati madai ya msingi mengi yametungiwa sheria ni kuupotosha umma. Kwamba kuna matukio ya utekaji, au watendaji kukimbia ofisi na wapinzani kuambiwa hawajui kusoma na kuandika, hizo ni hoja za kufanyia kazi badala ya kuweka blanketi lisilo na ufafanuzi eti No Reforms, No Election.
Sitanii. Nimepata shida kuwaelewa CHADEMA. Viongozi hawa wameshindwa kuwa na maridhiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameshindwa kuheshimu na kuridhiana na vyama vya upinzani, kwani wanatoa lugha za kejeli kwao kuwa ni vyama uchwara, mbaya zaidi wameshindwa kuridhiana ndani ya chama wamezalisha G55.
Nafahamu wengi wanadhani harakati zitafanya kazi. Kususia uchaguzi ni kosa la kihistoria kwa chama cha siasa. Ikiwa CHADEMA hawatapiga moyo konde wakaridhiana ndani kwa ndani wakaendelea na habari za kwamba wanaopinga msimamo wa sasa ni wafuasi wa “Mbowe” hakika watakumbuka shuka kukiwa kumekucha. Mkondo walioupitia NCCR-Mageuzi, CUF na kwa mbali TLP nauona ukivuma kuelekea CHADEMA.
Amkeni CHADEMA, rudini kwenye maridhiano. Shirikianeni na vyama vya upinzani wenzenu. Kama Nyerere alikwenda kuzungumza na wakoloni, ninyi mnashindwaje kuzunguza na Watanzania wenu walioko CCM? Kiburi si maungwana. Mnatuhumiwa kwa kiburi ndani na nje ya chama. Mnaweza kuwajaza upepo wanachama wenu mkasema liwalo na liwe, ila msiponisikiliza mtanikumbuka. Nenda kwenye meza ya mazugumzo. Zungumza na hao G55, zungumza na CCM. Miaka ya jino kwa jino, upanga kwa upanga iliishapita. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827