Abidjan, Ivory Coast – Katika jukwaa kubwa la viongozi wa taasisi za kibiashara barani Afrika, maarufu kama Africa CEO Forum, Tanzania imeendelea kujidhihirisha kama taifa linalochomoza kwa kasi kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Jumatatu, May 12, 2025, na kuhudhuriwa na zaidi ya wawekezaji 2,000, uligeuka kuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonyesha mafanikio yake, mikakati ya maendeleo, na dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa unaoshirikisha sekta binafsi kwa karibu.

Katika msafara ulioongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pamoja na viongozi wengine wakuu akiwemo Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, Tanzania iliwasilisha taswira mpya ya taifa linalofungua milango yake kwa wawekezaji wa ndani na nje, huku ikitangaza mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayoendelea nchini.

“Kikao chetu cha leo (jana) kikiwa na wawekezaji zaidi ya 2,000 ni nafasi adhimu kwetu kuwavutia, kuchukua mawazo yao na kuwafanya waijue Tanzania yetu,” alisema Bw. Mchechu, akisisitiza nafasi ya kipekee ambayo Tanzania imejijengea katika jukwaa hilo la kimataifa.

“Nchi zote zinapigania nafasi za kiuchumi. Tanzania kwa sasa ina mtaji mkubwa kutokana na msingi wa mahusiano na sera za kiuchumi zinazowekwa na viongozi wetu.”

Kwa mujibu wa viongozi wa Tanzania, vikao vya Africa CEO Forum si tu sehemu ya kujifunza, bali ni jukwaa la kuuza fursa za kiuchumi za Tanzania, hasa katika maeneo ya logistiki, madini, kilimo na fedha. Wameeleza kuwa ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kushiriki kwa bidii katika majukwaa haya ili kuwa mhimili wa mijadala ya maendeleo Afrika.

“Tunaamini kupitia mkutano huu, dunia inazidi kuijua Tanzania – sio tu kama nchi yenye utulivu wa kisiasa, bali kama taifa la fursa, la watu wenye vipaji, na la mazingira rafiki kwa biashara,” aliongeza Bw. Mchechu.

Mjadala mkuu wa mkutano huo ulilenga kuangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Katika hili, Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kwa kina jinsi Tanzania ilivyofanikiwa kufungua fursa za uwekezaji kwa kushirikiana kwa karibu na taasisi kama Shirikisho la Sekta binafsi Tanzania (TPSF) na Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI).

“Tanzania ni nchi inayoendelea kufungua milango kwa sekta binafsi – ya ndani na ya kigeni – kuwekeza. Ushirikiano huu unasaidia kuongeza uwezo wa uchumi wa ndani, na kuchangia huduma za kijamii kwa wananchi kupitia mapato ya serikali,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa ujumla, ushiriki wa Tanzania katika Africa CEO Forum unadhihirisha dhamira yake ya kujenga uchumi jumuishi, wenye ushindani wa kikanda na kimataifa, huku ikihamasisha uwekezaji, ubunifu na ushirikiano wa sekta zote.