Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu maalum wa Taifa utakaoandika historia mpya katika uendeshaji wa shughuli za chama hicho kikongwe barani Afrika.

Mkutano huo utafanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma, tarehe 29 na 30 Mei 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24 Jijini hapa kuhusu maandalizi ya Mkutano huo , Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo CPA Amos Makalla amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kwamba mkutano huo utakuwa wa kipekee na wa kihistoria kuliko yote iliyowahi kufanyika.

“Tunataka kufanya mikutano ya kihistoria,mkutano huu utakuwa bora na wa kipekee zaidi ya mikutano yote iliyopita,” amesema Makalla.

Kwa mujibu wa Makala,Mkutano Mkuu huo unatarajiwa kuwahusisha wajumbe takribani 2,000 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, pamoja na wageni waalikwa 700 wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali na mashirika ya ndani na nje ya nchi.

Aidha amesema Mkutano huo Mkuu utatanguliwa na vikao vya awali vya chama, vikiwemo Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa Mei 28,2025 ambavyo vitatoa mwelekeo na maandalizi ya ajenda kuu zitakazojadiliwa katika mkutano huo.

Makalla ametaja ajenda kuu zitakazojadiliwa kwenye mkutano huo kuwa ni Kupokea Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, pamoja na taarifa kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano,Uzinduzi Rasmi wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2025, itakayowasilisha dira ya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba na Marekebisho Madogo ya Katiba ya chama ili kuendana na mazingira na mahitaji ya sasa ya wananchi.

“Ilani ya uchaguzi ni mkataba kati ya chama na wananchi, Uzinduzi wake rasmi utaonesha dhamira na malengo ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu,ifahamike kuwa ilani ndio kitendea kazi cha kunadi Sera zetu,” amesema Makalla.

Sambamba na mkutano huo,amesema kutafanyika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Makao Makuu mapya ya CCM, itakayofanyika tarehe 28 Mei 2025 kuanzia saa tatu asubuhi, karibu na jengo la Jakaya Kikwete Convention Centre.

“CCM ina wanachama zaidi ya milioni 11. Ni muhimu kuwa na jengo la kisasa na lenye hadhi, linaloendana na ukubwa wa chama chetu,” amesema Makalla na ko ngeza;

“Tumefikia hatua ya kuwa na jengo litakalothibitisha uimara wa CCM kama chama kikubwa barani Afrika na Tanzania kwa ujumla,” amesisitiza.

Amos Makalla ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wanachama wote wa CCM kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano huu muhimu, akieleza kuwa utaratibu maalum umeandaliwa kwa ajili ya kuwapokea wajumbe na wageni wote watakaowasili Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo maalum.