Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
WAJUMBE Chama Cha Mapinduzi CCM Tawi la London Diaspora la Nchini Uingereza wametembelea Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kushuhudia shughuli za Baraza hilo ikiwemo uwasilishwaji wa miswada mbali mbali.
Wajumbe hao, wakiwa chini ya uongozi wa viongozi wakuu wa CCM kutoka Uingereza na Wanadiaspora zaidi ya 10, wakiongozwa na Mwenyekiti wa msafara huo Bw. Haruna Rajabu Mbeyu waishio London, ambapo mapema Juni 5, 2025 wamepata wasaha huo wa kutembelea Baraza hilo la Wawakilishi na kupata fursa ya kuteta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, Mhe. Ali Suleiman Ameir Mrembo ambaye amewakaribisha nyumbani ikiwemo kurudi kuchangamkia fursa za Uwekezaji.

Aidha, amewaambia kuwa, kwa Zanzibar Diaspora inamaana kubwa kwani wanachangia maendeleo ya Nchi yao ndo maana wanawatambua na wanapata masuala yote ya msingi.
“Kupitia Hadhi maalum, Serikali itahakikisha kila haki yako unapata. Hivyo kumbukeni nyumbani ni nyumbani mkumbuke ikifika muda murejee nyumbani, kwa wenye ujuzi kupitia vitengo vyetu vya Diaspora Serikali itahakikisha inafanya jambo maalum kama ni ajira ama mikataba ya kazi.
Muendelee kutuunga mkono, mkatusemehe mazuri Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Diaspora wa sasa mpo vizuri muendelee kututangaza kwenye Mataifa mliopo, sisi ni watu wa amani, na tuiendeleze amani yetu”. Amesema Mhe. Ali Suleiman Ameir.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa msafara huo, Bw Haruna Mbeyu amesema kuwa, wamefika visiwani Zanzibar kuendelea kujifunza mambo mbali mbali kwani Zanzibar wana kitengo kizuri na kikubwa cha Diaspora ambacho kimekuwa ni chachu kwa Wanadiaspora.
Wana Diaspora hao wapo Visiwani Zanzibar kuanzia Juni 3, 2025 Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na mahusiano kati ya wanadiaspora wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) sambamba na kujadili fursa mbalimbali za maendeleo na mchango wa Diaspora katika maendeleo kupitia Chama Cha Mapinduzi.


