Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma
Wiki iliyopita serikali imeleta furaha, matumaini na heshima kwa taifa letu. Nasema furaha, heshima na matumaini kwa nchi yetu si kwa jambo jingine, bali bajeti ya mwaka 2025/2026 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.
Bajeti hii si tu ya takwimu na mipango, bali ni dira ya kujinasua kiuchumi na kuelekea kwenye kujitegemea kwa asilimia 100 kama nchi. Rafiki yangu mmoja tulipotoka ukumbini pale bungeni akaniambia: “Hii si bajeti ya kawaida; ni bajeti ya maono, ujasiri na uthubutu wa kisiasa.”
Sitanii, kwa mara ya kwanza serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kupunguza utegemezi wa misaada ya kigeni. Mfano bora ni uamuzi wa serikali kulipia dawa za ARVs kwa wagonjwa wa ukimwi baada ya Marekani kutangaza kujiondoa kwenye ufadhili.
Miaka ya nyuma tulizoea kodi zinaongezeka kwenye mafuta na vinywaji, lakini hazikuwa na marengo mahsusi. Zamu hii serikali imeonyesha ujasiri wa hali ya juu na kusema sisi Watanzania tuwatibie wagonjwa wetu badala ya kusubiri misaada.
Nafahamu kuna watu wanaweza kujiuliza iwapo Marekani iliyotajwa kuwa inalipia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi tangu miaka ya 1980 imejitoa, sisi Tanzania tutaweza kweli kulipa gharama hizi? Serikali mbali na mpango wa awali wa kuanzisha kodi ya matibabu haya, imedhamiria kushirikiana na sekta binafsi kujenga viwanda vya dawa hapa nchini. Huu ni uamuzi sahihi na endelevu. Marekani wao wanafanya hivyo, sisi kwa nini tushindwe?
Kupanga ni kuchagua. Tulianza na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) – umeme ukasambaa kila kona ya nchi hii. Tukaja elimu, maji, sasa tumeshika afya. Ni wazi Rais Samia Suluhu Hassan anatupitisha katika mkondo sahihi. Ilipotajwa kuwa elimu itakuwa bure darasa la kwanza hadi kidato cha sita, miguno ilikuwa mingi. Uhalisia ni kwamba Rais Samia ameliweza hili na linaendelea kwa ufanisi mkubwa.

Sitanii, bajeti hii pia imegusa maisha ya kila Mtanzania. Bei ya mitungi ya gesi imepunguziwa kodi, hatua ambayo itawapunguza mzigo wa gharama ya maisha wananchi wengi, hasa wa kipato cha chini. Umeme sasa utasambazwa hadi vitongoji vyote, huku maji yakitarajiwa kufika hadi mlangoni kwa maeneo ya vijijini. Flyover ya Mwenge, barabara mpya, pamoja na miradi ya SGR kuelekea Mwanza na Kigoma – haya yote ni ishara kuwa serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu kwa kasi ya kweli.
Kwa waendesha bodaboda na wafanyabiashara wadogo, kuna afueni kubwa kupitia utoaji wa leseni ambazo zimeshushwa kutoka Sh 70,000 hadi Sh 30,000 na kufutiwa kodi ya Sh 65,000. Kwa wafanyabiashara nao ni kicheko. Kufunga biashara kiholela sasa basi. Kupitia bajeti hii hakuna taasisi yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kufunga biashara ya mtu isipokuwa kwa kibali cha waziri mwenye dhamana. Katika bajeti hii, serikali imesikiliza kilio cha wananchi na kuchukua hatua madhubuti.
Wastaafu wamepata faraja baada ya serikali kutangaza ongezeko la pensheni kwa asilimia 150. Hii ni heshima kwa wazee waliolitumikia taifa kwa uaminifu. Katika sekta ya viwanda, serikali imepanga kujenga kongani za viwanda kila wilaya. Hili si jambo dogo. Ni hatua ya kuleta mapinduzi ya viwanda, kuimarisha ajira, kuongeza mapato ya ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya bandari, pamoja na kurejesha asilimia 51 ya mapato kwa TANAPA na Ngorongoro, ni dalili kuwa rasilimali za taifa zinaanza kutumika kwa masilahi ya Watanzania. Serikali pia imepanga kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma kwa mabomba mawili – la maji safi na la umwagiliaji. Huu ni mkakati wa kuimarisha usalama wa chakula na ustawi wa wakulima.

Katika sekta ya madini, mpango wa kupanua survey kutoka asilimia 16 hadi 50 ni hatua ya kijasiri itakayoongeza tija ya matumizi ya rasilimali. Hii ni bajeti ya uchaguzi, lakini tofauti na ilivyozoeleka, bajeti hii inaelekeza nguvu katika maendeleo ya watu. Lakini pia, Tanzania kwa mara nyingine kupitia bajeti hii itagharamia yenyewe uchaguzi wote wa mwaka 2025. Nchi zilizoendelea zinafanya hivi.
Sitanii, bajeti hii inaonyesha ukweli kuwa sasa tuna nafasi ya kuweka historia mpya kama taifa. Serikali imeonyesha njia, jukumu letu ni kuichambua bajeti hii kwa jicho la matumaini na uhalisia. Tanzania sasa inaandika ukurasa mpya wa historia – kutoka nchi tegemezi kwenda taifa huru kiuchumi. Taifa linaamka, nasi hatupaswi kulala. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827