Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia na Habari, Jerry Silaa (Mb), ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupiga kambi katika kiwanda cha kutengeneza simu janja cha Raddy Electronics kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani, kwa lengo la kufuatilia kwa ukaribu ubora na viwango vya uzalishaji kulingana na ushindani wa soko, ili kudhibiti uwepo wa simu feki nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua viwanda vinavyomilikiwa na mwekezaji mzawa, Ramadhani Hassani Mlanzi, ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing Ltd na Raddy Electronics, Silaa amesema TCRA ina mamlaka ya kusajili vifaa vya kielektroniki na ina maabara maalum kwa ajili ya kufanyia tathmini ya vifaa hivyo.

“Ninaelekeza TCRA waje hapa, watushauri kwa maamuzi sahihi bila haraka, kwa kushirikiana na wadau wote, Simu nyingi zinazotumiwa na wananchi ni feki – unaweza kuona simu nzuri lakini haishiki mtandao, Ni muhimu kuwa na utaratibu mzuri wa kutambua aina ya vifaa vinavyotengenezwa nchini, gharama zake, na viwango vya ubora ili kuwa na Taifa linaloweza kujivunia bidhaa zake,” alisema Silaa.
Aidha, Waziri Silaa ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufanya kazi kubwa ya kuimarisha miundombinu ya mawasiliano.
Amebainisha kuwa minara 758 ya mawasiliano imejengwa na mingine 636 inaendelea kujengwa nchi nzima.
Vilevile, mkongo wa Taifa wa mawasiliano tayari umeenea kote nchini na umeunganisha Tanzania na nchi jirani kama Uganda, Malawi, Kenya, Mozambique, na juhudi zinaendelea kuunganisha na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika hatua nyingine, Waziri Silaa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara na timu yake kuandaa andiko maalum litakalomshauri kuhusu mahitaji ya nyaya za fiber nchini, likihusisha makampuni yote yanayosambaza huduma za mawasiliano kupitia fiber optic. Amesisitiza kuwa:
“Sihitaji kufanya maamuzi haraka bila ushauri wa kitaalamu.”
Silaa pia ameeleza kuwa serikali inalenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote ili waweze kunufaika na TEHAMA katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.
Kuhusu changamoto za kikodi zinazolikabili kiwanda cha Raddy Electronics, aliahidi kuzichukua na kuziwasilisha kwa mamlaka husika za serikali ili kuona namna bora ya kuzitatua.

Kwa upande wake, mwekezaji Ramadhani Hassani Mlanzi ameeleza kuwa kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing Ltd kilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2021.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha hadi kilomita 24,000 za nyaya za optic fiber kwa mwaka, na kinatarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 5,000.
Naye Meneja wa Mauzo na Masoko wa kiwanda hicho, Fredrick Mtui, ameeleza kuwa kiwanda cha simu janja tayari kimekamilika kwa asilimia 100, na tayari kimeanza uzalishaji wa awali wa simu 2,500.
Ameongeza kuwa, mara baada ya uzinduzi rasmi na mzunguko wa soko kuimarika, kiwanda hicho kitapata uwezo wa kuzalisha hadi simu 9,000 kwa siku, sawa na 270,000 kwa mwezi.



