Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Benki ya CRDB imehitimisha rasmi kampeni yake ya “Fainali Ndiyo Mpango” kwa kushirikiana na TemboCard, huku washindi mbalimbali wakijinyakulia zawadi zenye thamani kubwa ikiwemo televisheni za kisasa (Smart TV) na safari ya kwenda kushuhudia mechi za Kombe la Dunia la FIFA 2026 zitakazofanyika nchini Canada, Marekani na Mexico.

Akizungumza leo Juni 11,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa droo ya mwisho ya kampeni hiyo, Meneja Mwandamizi Kitengo cha Kadi Karingtoni wa CRDB amesema kampeni hiyo imelenga kuwazawadia na kuwathamini wateja wanaotumia TemboCard katika kufanya miamala mbalimbali ya kifedha.

“Washindi wanakwenda kutazama Kombe la Dunia Fifa 2026 Godfrey Hezekiah Chibulunje ,Habibi Sarah Filikunjombe,Lenah Gacher Manyua”amewataja Meneja

Amesema katika droo zote ya mwisho ya kampeni hiyo, jumla ya washindi 20 wamepatikana na kujishindia zawadi mbalimbali, huku baadhi yao wakipata fursa ya kipekee ya kusafiri kwenda kushuhudia michuano ya Kombe la Dunia 2026, tukio ambalo linatarajiwa kuvutia mamilioni ya mashabiki wa soka duniani.

Mbali na safari hiyo ya kihistoria, washindi wengine wamejishindia Smart TV zenye ukubwa wa inchi 85 pamoja na zawadi nyingine zilizotolewa katika kipindi chote cha kampeni.

CRDB imeeleza kuwa kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali na TemboCard, huku ikichochea utamaduni wa matumizi ya mifumo rasmi ya malipo miongoni mwa wateja wake.

Benki hiyo imewashukuru wateja wote walioshiriki kampeni hiyo na kuahidi kuendelea kuandaa promosheni na kampeni mbalimbali zitakazoongeza thamani kwa wateja pamoja na kuboresha uzoefu wao wa huduma za kifedha.