
Wakulima wa zao la pamba kutoka vijiji vya Mbutu, Iyogelo, Ilambakuki, Imalanguzu na Mwamakoma vilivyopo katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora, wamehamasika kufungua akaunti za benki na kusajili laini za simu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupokea malipo ya mazao yao kwa njia ya kidijitali. Hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi, usalama na uharaka wa malipo kwa wakulima.
Wakulima hao wamefungua akaunti kupitia Benki ya NMB pamoja na kusajili laini kupitia mtandao wa simu wa Mixx by Yas, hatua itakayowawezesha kupokea fedha zao kwa urahisi kupitia mifumo ya benki na huduma za kifedha za simu za mkononi.
Zoezi hilo limefanyika kwa kushirikiana na AMCOS za Ngw’ajojabi, Ngw’asabi na Mwamakoma AMCOS, likitekelezwa kufuatia waraka wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika unaoelekeza malipo ya wakulima wa pamba kufanyika kupitia akaunti za benki na huduma za fedha kwa njia ya simu badala ya kutegemea fedha taslimu. Lengo ni kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kwa wakati, kwa uwazi na kwa usalama zaidi.
Mwitikio wa wakulima umeendelea kuongezeka siku hadi siku kufuatia juhudi za uhamasishaji zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali. Hadi kufikia Juni 10, 2026, jumla ya wakulima 506 wamejitokeza na kufungua akaunti pamoja na kujiunga na huduma za kifedha za simu, hatua inayoonesha uelewa na utayari mkubwa wa wakulima kupokea mabadiliko ya mfumo wa malipo ya kidijitali.
Aidha, uhamasishaji wa zoezi hilo umefanywa na Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Tabora, Peja Mhoja pamoja na Mrajis Msaidizi (Uhamasishaji), Ibrahim Kadudu, ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wakulima kujiunga na mifumo rasmi ya kifedha ili kunufaika na malipo ya kisasa, salama na yenye tija.












